Huenda wakulima watakuwa na uhakika wa soko la tumbaku baada ya wanunuzi kuongeza kiasi watakachonunua mwaka ujao wa kilimo.
Kampuni ya Japan Tobacco Incorporation (JTI) imeahidi kununua kilo milioni 30 za tumbaku kutoka kwa wakulima katika msimu ujao wa kilimo.
Ahadi hiyo imetolewa jana (Septemba 26, 2022) na Rais na Mtendaji Mkuu wa JTI, Masamichi Terabatake mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyetembelea ofisi za kampuni hiyo nchini Japan.
Majaliwa amesema uamuzi wa kampuni hiyo kuongeza kiwango cha ununuzi wa tumbaku utatoa ahueni kwa wakulima wa Tanzania ambao walikuwa hawana uhakika wa soko la zao hilo.
“Leo Bodi ya Wakurugenzi (ya JTI) imetangaza uamuzi wa kununua kilo milioni 30 za tumbaku kutoka kilo milioni 14 ambazo walinunua msimu uliopita,” amesema Majaliwa.
Mara baada ya kutangazwa kwa neema hiyo Waziri Majaliwa amesema ununuzi huo wa tumbaku utakaofanywa kwenye msimu ujao ni fursa kubwa kwa wakulima wa Tanzania kuzalisha zaidi kwani kiasi kinachohitajika ni zaidi ya uzalishaji unaofanyika.
“Miaka ya nyuma makampuni yaliyokuwa yakinunua tumbaku yalizoea kuwapangia wakulima wetu idadi ya kilo za kununua, kwa hiyo hata uzalishaji haukuwa mkubwa sana,” amesema Waziri Majaliwa.
Sambamba na hilo majaliwa amewataka wakulima wakulima kuzalisha zao hilo kwa wingi ili kuweza kufikia mahitaji yanayohitajika sokoni.
“Kwa hiyo wakulima sasa waongeze uzalishaji ili tufikie lengo hili,” amesisitiza Majaliwa.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021 kinachotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), mauzo ya tumbaku nje yalipungua kwa asilimia 14.3 na kufikia Dola za Marekani milioni 127.5 (Sh293 bilioni) kwa mwaka 2021 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 148.7(Sh342 bilioni) kwa mwaka 2020.
Upungufu huo ulichangiwa na kupungua kwa kiasi cha tumbaku kilichouzwa nje kutoka tani 42,600 mwaka 2020 hadi tani 37,700 mwaka 2021.
Hata hivyo, wastani wa bei ya tumbaku katika soko la dunia iliongezeka kwa asilimia 1.3 hadi Dola za Marekani 3,538.4( Sh8.1 milioni) kwa tani mwaka 2021 ikilinganishwa na dola za Marekani 3,494.2(Sh8 milioni) kwa tani mwaka 2020.