Waziri Ummy: Bima ya Afya ni hiari siyo lazima

HomeKitaifa

Waziri Ummy: Bima ya Afya ni hiari siyo lazima

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ikipita itahakikisha wananchi wanapata huduma bila kikwazo lakini hakuna mtu atakayelazimishwa kuwa na bima hiyo kwa sababu itakuwa ni hiari.

Muswada wa sheria hiyo uliwasilishwa bungeni kwa mara ya kwanza Septemba 23, 2022 ambapo utajadiliwa katika kamati kabla ya kumalizia mchakato mwingine wa utungaji wa sheria.

Waziri Ummy aliyekuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 27, 2022 amesema bima hiyo itakuwa ni hiari siyo lazima.

Waziri wa Afya , Ummy Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari.

“Hakuna mtu atakayepigwa faini, atakayefungwa au kubughuziwa kwa namna yoyote ile kisa hatakua na bima ya afya. Bima ya afya ni hiyari,” amesema Waziri Ummy.

Amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila kikwazo na kwa gharama nafuu.

“Tutaendelea kuelimisha kuwa lengo la Serikali kupitia bima hii ni kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi,” amesema Ummy ambaye ni Mbunge wa Tanga Mjini.

Ili kuhakikisha sheria hiyo inatekelezeka vizuri, utawekwa utaratibu wa kuchangia kwa kuzingatia kaya, na mtu mmoja mmoja asiye katika kaya ambapo bima hiyo itakuwa na kitita cha msingi na vifurushi mbalimbali vitakavyowezesha wananchi kuchagua kulingana na mahitaji.

“Kwa wasio na uwezo Serikali itatumia utaratibu wa TASAF(Mfuko wa Maendeleo ya Jamii) kuwatambua kwa ajili ya kuwapa huduma. Wananchi hawatalazimishwa kujiunga na mfuko mmoja, watakua wa na uhuru wa kuchagua skimu za bima zilizosajiliwa kwa mujibu wa sheria,” amesisitiza Ummy.

Amesema malipo ya bima yanaweza kuwekewa utaratibu wa kulipwa kwa awamu kulingana na uhitaji wa wateja na watoa huduma.

Akizungumzia kufungamanisha na baadhi ya huduma za kijamii ni kuongeza msukumo wa watu kuchangamkia fursa hiyo ya kuwahakikishia afya zao.

“Kufungamanishwa kwa baadhi ya huduma za kijamii kunatarajia kuweka msukumo kwa wananchi ili wachukue hatua za kujiunga na bima ya afya ili kuepuka changamoto ya kutopata huduma za afya bila kikwazo cha fedha,” amesema Waziri Ummy.

Waziri Ummy amesema Serikali inatarajia kufungamanisha umiliki wa kadi ya bima ya afya kwa wote na upatikanaji wa huduma zilivyofungamanishwa na umiliki wa kadi au Namba ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA).

error: Content is protected !!