Mapato yatokanayo na shughuli za uwindaji wa kitalii nchini Tanzania yameongezeka zaidi ya mara mbili ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, huku yakitazamiwa kuongezeka zaidi miaka ijayo.
Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2021 kilichotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kinaeleza kuwa uwindaji wa kitalii uliingizia Tanzania Sh35.7 bilioni mwaka 2021.
Mapato hayo yameongezeka kwa asilimia 130.3 kutoka Sh15.5 bilioni yaliyorekodiwa mwaka 2020.
NBS katika kitabu hicho inaeleza kuwa hali hiyo imechangiwa na ongezeko la idadi ya wawindaji wa kitalii kutoka 251 mwaka 2020 hadi 548 mwaka jana.
Tangu mwaka 2015 idadi ya wawindaji wa kitalii imekuwa ikipanda na kushuka ikilinganishwa na mchango wake kwenye pato la Taifa GDP.
Mathalan, mwaka 2015 idadi ya wawindaji wa kitalii ilikiwa 608, mwaka uliofuata ikapungua hadi 495 na mwaka 2017 ikapungua zaidi hadi 473.
Mwaka 2018 idadi iliongezeka hadi 503 na mwaka uliofuata idadi yake ikaongezeka hadi 519 kabla haijaporomoka zaidi hadi wawindaji wa kitalii 251 mwaka 2020.
Sababu kuongezeka kwa shughuli za wawindaji wa kitalii
Kuongezeka kwa idadi ya watalii wa Kimataifa nchini kumehuisha shughuli za uwindaji wa kitalii Tanzania.
Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dk Pindi Chana katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/23, amesema kuwa mwaka jana idadi ya watalii wa kimataifa waliotembelea Tanzania ilikuwa 922,692 ikiwa ni ongezeko la asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 wa mwaka juzi.
Pia kupungua kwa matukio ya ujangili, uwindaji na uvunaji haramu wa maliasili kumesaidia kuimarisha sekta ya utalii nchini baada ya Serikali na wadau kuwekeza nguvu kubwa kudhibiti vitendo hivyo.
Waziri Dk Chana amesema kuwa wizara yake mwaka 2021/22 imeongeza operesheni maalum za kiintelijensia zilizozuia matukio 66 ya ujangili, kukamatwa kwa silaha mbalimbali zikiwemo bunduki 135 na kuvunjwa kwa mitandao ya ujangili nchini Tanzania.
Uwindaji wa kitalii huusisisha shughuli za kuwinda na upigaji picha wanyamapori.