China haifungui kituo cha polisi Tanzania

HomeKimataifa

China haifungui kituo cha polisi Tanzania

Watanzania wametakiwa kupuuzia taarifa iliyotolewa na idhaa ya kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa  nchi ya China ina mpango wa kufungua kituo cha polisi barani Afrika ikiwemo Tanzania.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amekanusha madai hayo kwa kueleza kuwa taarifa hiyo iliyonukuliwa kutoka baadhi ya vyombo vya habari nchini Nigeria siyo ya kweli bali ina lengo la kuleta sintofahamu.

“Niwahakikishie hizi ni habari za uongo. Sisi kama Tanzania hatuna mkataba wowote wa mahusiano ya ushirikiano wa kipolisi ambao unapelekea kufungua vituo vya polisi kama ilivyodaiwa, hatujaomba wala wao hawajatuomba,” amesema Kairuki.

 

View this post on Instagram

 

A post shared by Maelezo News (@maelezonews)

Balozi  Kairuki amesisitiza kuwa ni kweli upo utaratibu wa nchi moja kufungua kituo cha polisi kwenye taifa lingile lakini lazima kuwe na makubaliano maalum baina ya mataifa hayo kwa madhumuni mahususi.

“China ina makubaliano na nchi ya Italia ya polisi wake kufanya kazi katika nchi hiyo na dhumuni lake lilikuwa kukidhi mahitaji ya maelfu ya watalii wa China waliokuwa wanaenda kutalii katika jiji la Milan,” amesema.

Aidha Kairuki amesikitishwa na kitendo cha BBC kutumia vyanzo visivyo vya kuaminika kuandika habari zake jambo ambalo linashusha heshima ya shirika hilo kongwe duniani.

Taarifa  iliyochapishwa katika tovuti ya BBC na ukurasa wa mtandao wa Twitter  siku ya jumanne Oktoba 18 mwaka huu ilieleza China imekuja na mpango huo ili kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na raia wake katika nchi za Tanzania, Nigeria na Lesotho.

error: Content is protected !!