Chama cha Demokrasia (CHADEMA) mkoa wa Singida kimesema kimechoka kumwona Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu akiishi ughaibuni kama mkimbizi, hivyo kuitaka serikali kumhakikishia usalama wake ili arejee nchini.
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Singida, Emmanuel Jingu, alitoa kauli hiyo jana alipofunga kikao cha viongozi wa majimbo chenye lengo la kujadili mustakabali wa chama kuelekea uchaguzi wa ndani wa chama pamoja na uandikishaji wa wanachama kwa mfumi wa kidigitali.
“Tunatoa rai kwa serikali imhakikishie usalama Lissu arudi nchini maana anaishi ughaibuni kama mkimbizi, tumechoka mtu wetu kuwa mkimbizi huko, serikali itoe tamko Lissu arudi,” alisema.
Jingu alisema chama kinapata athari kutokana na Lissu kuendelea kuishi nje kwa kuwa ni Makamu Mwenyekiti wa chama, hivyo kuwapo kwake nchi kutakisaidia chama.
“Wananchi wana shauku ya kumwona Lissu hasa ikizingatia alikuwa mgombea Urais mwaka 2020 na wanataka kujua nini kitafuata kama atarudi tena ulingoni 2025 au hataki, anapumzika au atarudi jimboni, sasa yeye akirudi ndiye aje awaeleze wananchi,” alisema Jingu.