Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amesimikwa rasmi kuwa Mkuu Mpya wa Chuo Kikuu cha Iringa akichukua nafasi ya Askofu Mstaafu Elinaza Sendoro aliyemaliza muda wake baada ya kuhudumu katika nafasi hiyo kwa miaka mitatu.
Tukio hilo limefanyika jana katika mahafali ya 25 ya chuo hicho yaliyofanyika chuoni hapo mjini Iringa huku zaidi ya wahitimu 1900 wakitunukiwa vyeti vyao katika fani mbalimbali.
Akizungumza mara baada ya kusimikwa, Jenerali Mabeyo ameushukuru uongozi wa taasisi hiyo kwa kumpa nafasi hiyo muhimu kwa maendeleo ya elimu nchini huku akiahidi kushirikiana na uongozi na wadau wake wote kukitangaza vyema chuo hicho.
“Nashukuru kwa heshima hiyo mliyonipatia, nimeipokea na nimuombe mwenyezi Mungu aniongoze ili niweze kuwatumikia vyema wanajumuiya wa chuo hiki kwa manufaa ya jamii yote ya watanzania,” alisema Mabeyo.
Baada ya kupewa wadhifa huo, Jenerali Mabeyo naye amemteua Meja Jenerali Paul Kisesa kuwa mjumbe wa baraza la Chuo hicho.