Rais Samia Suluhu Hassan ameungana na viongozi mbalimbali duniani kuomboleza vifo vya zaidi ya watu 3,500 waliofariki dunia baada ya kutokea kwa tetemeko nchini Uturuki na Syria.
Wizara ya Afya ya Uturuki imethibitisha vifo 2,379 huku Syria ikirekodi vifo zaidi ya 1,400.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa huenda waliokufa ni mara nane zaidi ya idadi inayojulikana hivi sasa.
Serikali ya Uturuki imepeleka magari ya kubebea wagonjwa takriban 813 katika maeneo yaliyoathirika, na vikundi maalumu vya huduma za dharura zaidi ya 220 vimeambatana na magari hayo.
Tetemeko lenye ukubwa wa 7.8 kwenye kipimo cha Richter liliitikisa sehemu ya katikati mwa Uturuki na kaskazini mwa Syria alfajiri ya jana, likiharibu vibaya miundombinu katika miji 12 katika nchi hizo.
Kufuatia tetemeko hilo ambalo limeacha majonzi na vilio, Rais Samia ametoa salamu zake za rambirambi kwa wananchi na viongozi wa nchi hizo.
“Kwa niaba ya Serikali na wananchi wa Tanzania, natoa pole kwa wote waliofikwa na msiba huu. Mawazo na maombi yetu yako pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu,” ameandika Rais Samia katika ukurasa wake wa Twitter.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu (OCHA) imesisitiza kwamba tetemeko la awali la kipimo cha Rishta 7.8 lilipiga katika kilele cha majira ya baridi.
Kitovu cha tetemeko hilo kilikuwa kusini mwa Türkiye, ambapo ni karibu na Gaziantep kituo muhimu cha misaada cha Umoja wa Mataifa kaskazini mwa Syria na hivyo kituo hicho kuwa miongoni mwa miji iliyoathiriwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema amesikitishwa sana na taarifa kuhusu hasara kubwa ya kupotea kwa maisha ya watu iliyosababishwa na tetemeko hilo.
“Moyo wangu unawaendea watu wa Uturuki na Syria katika saa hii ya msiba mkubwa. Natuma salamu zangu za rambirambi kwa familia za waathirika na kuwatakia ahueni ya haraka wote waliojeruhiwa.
“Umoja wa Mataifa umejitolea kikamilifu kuunga mkono hatua za uokozi na kuwasaidia wenye uhitaji. Timu zetu ziko huko kutathmini mahitaji na kutoa msaada,” amesema Guaterres.