Pacha aliyebaki afariki

HomeKitaifa

Pacha aliyebaki afariki

Pacha aliyesalia ‘Rehema’ kati ya mapacha wawili waliotenganishwa Julai Mosi mwaka huu, amefariki dunia jana saa 5 asubuhi Agosti 11, wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Rehema amefariki dunia siku 32 baadaye tangu kifo cha pacha wake ‘Neema’ kilichotokea Julai 10 mwaka huu.

Neema alifariki dunia baada ya hali yake kubadilika ghafla akiwa ICU. Pacha huyo alizikwa Julai 14 katika makaburi ya Ulongoni B yaliyopo Gongo la Mboto.

Akizungumza  leo Agosti 12, 2022 Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kwa umma, Muhimbili, Aminiel Aligaesha amethibitisha kutokea kwa kifo hicho. “Ni kweli Rehema alifariki jana.”

Bibi wa Pacha hao Dorica Josiah amesema amepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa kwani hali ya mtoto huyo ilikuwa ikiendelea vizuri lakini siku chache nyuma ilibadilika ghafla baada ya kupata shida ya mapafu.

Pacha hao Rehema na Neema walitenganishwa Julai Mosi mwaka huu upasuaji uliofanyika kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa afya 31 kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Ireland wanaotokea Shirika la Operation Child Life.

Awali Dk Zaitun Bokhari aliyeshiriki katika operesheni ya kuwatenganisha, alisema ugumu mkubwa ulikuwa katika kutenganisha ini ambalo liliungana na baadhi ya mishipa mikubwa ya ini ilikuwa imeungana pia.

“Ini ilikuwa changamoto kubwa lakini pia ngozi inayofunika moyo ilikuwa imeungana na kufanya kitu kimoja. Ilibidi ngozi ifumuliwe ili iweze kutenganishwa kwa ini na moyo pia. Tumefanikiwa kuwatenganisha na kila mtoto amebaki na ini lake na mishipa inayobaki kwenye ini wamebaki nayo kila mmoja,” alisema alipokuwa akieleza mafanikio ya operesheni hiyo.

Watoto hao walizaliwa kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa na kuletwa Muhimbili Novemba mwaka jana, wakiwa na uzito wa kilo saba na sasa wana uzito wa kilo 13.3.

SOURCE: MWANANCHI

error: Content is protected !!