ACT- Wazalendo wataka mfumo wa Air Tanzania kufumuliwa

HomeKitaifa

ACT- Wazalendo wataka mfumo wa Air Tanzania kufumuliwa

Chama Cha ACT-Wazalendo kimeitaka Serikali kubadili haraka mfumo wa uendeshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili kuliepusha na hasara ambayo imekuwa ikiripotiwa kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.

Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo Zitto Kabwe, amewaeleza wanahabari wakati akiwasilisha uchambuzi wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ( CAG) leo Apirili 10 2023, kuwa mfumo wa sasa unaowalazimu ATCL kukodi ndege kutoka kwa Wakala wa Ndege wa Serikali (TGFA) ndio chanzo cha hasara kwa shirika hilo.

“Mfumo uliopo sasa ATCL haimiliki ndege. Ndege zote zilizonunuliwa na Serikali kwa fedha za walipa kodi zinamilikiwa na TGFA na kukodishwa kwa ATCL. Tunapendekeza ATCL imilikishwe ndege zote inazo kodishiwa kutoka TGFA,” amesema Zitto jijini Dar es Salaam.

Zitto amebainisha kuwa mwaka 2022 ATCL ilitakiwa kuilipa TGFA Sh63 bilioni kama gharama ya ukodishaji ndege, hivyo kuondolewa kwa utaratibu huo kutalipatia ahueni shirika hilo la ndege.

Kwa mujibu wa CAG, kwa mwaka 2021/22 ATCL ilirekodi hasara ya Sh35.23 bilioni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kuingia gharama mara mbili ya malipo ya ukodishaji ndege na gharama za matengenezo kwa TGFA ambapo kama zisingekuwepo hasara ingepungua mpaka Sh9.85 bilioni.

error: Content is protected !!