Wakimbizi Tanzania kuanza kuhakikiwa

HomeKitaifa

Wakimbizi Tanzania kuanza kuhakikiwa

Serikali ya Tanzania imesema itaanza uhakiki wa wakimbizi na waomba hifadhi kutoka nchi jirani ili kuwarejesha makwao wasiostahili na kuongeza usalama nchini.

Tanzania ni miongoni mwa nchi katika ukanda wa Afrika Mashariki zinazohifadhi kiwango kikubwa cha wakimbizi na waomba hifadhi kutoka nchi za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) waliokimbia machafuko nchini mwao.

Katika hotuba yake Januari 22, 2024 jijini Dar es Salaam, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali yake itafanya uhakiki huo baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lililokuwa likifanya kazi ya kurudisha wakimbizi katika nchi zao “kuishiwa nguvu”.

“Tumefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na lile Shirika la kuhudumia Wakimbizi Duniani lakini ukweli ni kwamba lile Shirika limeishiwa nguvu na ule moto wa kurudisha wakimbizi sasa umepungua,” amesema Rais Samia wakati wa mkutano wa saba wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF) na makamanda.

Rais Samia amebainisha kuwa baada ya zoezi la uhakiki Serikali itazungumza na nchi wanazotoka wakimbizi na waomba hifadhi hao ili kutafuta njia ya kuwarudisha.

“Kama mlivyosema wengine siyo wakimbizi wanaishi kama raia na wanajiona kama ni Watanzania kwa hiyo hili kama angalizo tumelichukua na tutakwenda kulifanyia kazi,” ameeleza Rais Samia.

Hata hivyo, Rais Samia hakuweka bayana uhakiki huo utaanza lini na zoezi la kuwarejesha litaanza lini.

Miaka ya hivi karibuni Tanzania kwa kushirikiana na UNHCR imekuwa ikiwarejesha nyumbani wakimbizi wengi baada ya hali kwenye nchi zao kutulia. Hadi Mei 2023 wakimbizi 10,335 walirejeshwa makwao katika nchi za Burundi, Marekani, Canada, Ufaransa na Australia kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Kwa Mujibu wa  Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda, Kuanzia Januari 1 hadi Disemba 31, 2023 Tanzania ilipokea waomba hifadhi 138,149 wanaotoka katika nchi za Rwanda, Burundi na DRC.

Jenerali Mkunda amewaambia wahudhuriaji wa mkutano huo kuwa baada ya kufanya mahojiano wamegundua kuwa baadhi ya waomba hifadhi, wamekimbia nchi zao kutokana na ugumu wa maisha na sio sababu za kiusalama kama walivyobainisha.

“Ni maoni yetu kwamba kuendelea kuwepo kwa wakimbizi hao na waomba hifadhi hao kwa muda mrefu ni tishio la usalama kwani kwa taarifa zilizopo ni kwamba baadhi ya waomba hifadhi  hao au wakimbizi au familia zao wameajiriwa serikalini kwa nafasi mbalimbali na wengine wamepewa teuzi kwa nafasi mbalimbali zenye maamuzi,” amesema Jenerali Mkunda.

error: Content is protected !!