Karibuni serikali ya Denmark imetangaza kuwa itafunga ubalozi wake nchini Tanzania ifikapo mwaka 2024.
Serikali ya Tanzania kupita Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula imeonesha kusikitishwa na hatua hiyo ya Denmark.
Kikubwa cha kufahamu ni kuwa Ubalozi wa Denmark haijafungwa kwa skendo za kijasusi, vita ya kibiashara, kiuchumi au jambo lolote baya baina ya Tanzania na Denmark. Serikali ya Denmark imesema itafunga ubalozi huo ili kujielekeza zaidi katika kufanya kazi na nchi zenye machafuko na migogoro.
Ubalozi hufungwa endapo malengo husika ya kufungua ubalozi yametimia. Lakini pia vita na machafuko yanaweza kupelekea kufungwa kwa ubalozi, swali, Tanzania ina vita, au machafuko? Jibu ni hapana.Denmark ilifungua ubalozi wake mnamo 1963, lakini je, malengo ya kufungua ubalozi wake hapa nchini yametimia? Hapa jibu yawezekana kuwa Tanzania tayari imeingia katika uchumi wa kati hivyo Denmark ikaona kuwa haina haja kuwa balozi tena nchini na sasa wanataka kusaidia nchini nyingine.
Na sio lazima kabisa kuwa na ubalozi nchi fulani ndio itoe tafsiri ya uhusiano baina ya nchi hizo, bado nchi moja inaweza kuwa na uhusiano bila hata kuwa na muwakilishi wa moja kwa moja kwenye nchi husika. Katika dunia hii ya utandawazi dunia inaelekeza nguvu kwenye Diplomasia ya Kidijitali (Digital Diplomacy) ambapo zipo nchi zina mahusiano tayari yakidijitali pasi na kuwa na uwakilishi wa moja kwa moja.
Marekani imefungua ubalozi wa aina hii Tehran nchini Irani, lakini pia mataifa makubwa kama Uingereza, Sweden, Ufaransa na Poland zimejielekeza katika kutumia diplomasia hii (virtual diplomacy). Hii inasaidia kupunguza matumizi makubwa ya Serikali na kuelekeza nguvu kwenye mambo ya msingi zaidi.
Uhusiano wa Tanzania na Denmark bado utakuwa imara, japo ubalozi utafungwa.