Agizo la Makamba kwa wakuu wa Mikoa 8

HomeKitaifa

Agizo la Makamba kwa wakuu wa Mikoa 8

Akizungumza kwenye semina iliyowakutanisha wakuu wa mikoa minane jijini Tanga, pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali, bunge, wizara ya nishati na taasisi zake, Waziri wa Nishati, January Makamba ametoa agizo kwa viongozi hao kuhakikisha utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika linalopita kwenye mikoa hiyo unafanikiwa.

Makamba amewataka wakuu hao wa mikoa kuimarisha ulinzi na usalama kwenye maeneo yao kwa kile alichoeleza kuwa ndio sababu moja wapo ya bomba hilo kupita nchini na pia kuhakikisha fursa zitakazopatikana zinanufaisha wananchi wa mikoa yao.

“Moja ya sababu za bomba hili kupita nchini kwetu ni uhakika wa ulinzi na usalama uliopo. Usalama huo utaendelea kuwepo kama wanaosimamia usalama huo kwenye maeneo linapopita bomba wana uelewa kuhusu mradi na kile kinachohitajika kufanywa, ili walioamua bomba hili lipite kwetu wawe na imani kwamba walifanya uamuzi sahihi,” alisema Makamba.

Semina hiyo itakayofanyika jijini Tanga kwa siku tatu inalenga kutengeneza uelewa mpana kwa viongozi hao kuhusu mradi na kujadili fursa mbalimbali zitakazopatikana katika utekelezaji wake.

error: Content is protected !!