Serikali yajivunia mafanikio na miradi ya maendeleo Katavi

HomeUncategorized

Serikali yajivunia mafanikio na miradi ya maendeleo Katavi

Katavi, Tanzania – Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kudumisha usalama na utulivu ndani ya mipaka yake, huku ikijivunia mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Katika ziara yake mkoani Katavi, Rais Samia Suluhu alitoa taarifa juu ya hali ya nchi na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha ustawi wa wananchi.

“Nchi yetu iko shwari, mipaka yote ya nchi yetu iko salama na tunaendelea kudumisha ushirikiano na majirani zetu wote,” alisema Rais Samia. Aliongeza kuwa kupitia falsafa ya 4R inayoielekeza serikali kusimamia maridhiano, mageuzi, na ujenzi mpya wa taifa, hali ya kisiasa nayo iko shwari. Vyama vya siasa vinaendelea na shughuli zao kwa amani na nchi inazidi kudumisha umoja na ustahamiliana.

Kwa upande wa uchumi, Rais Samia amesema maendeleo makubwa ni kutokana na usimamizi mzuri wa sera za uchumi, biashara, na uwekezaji. “Tunakwenda vizuri ikiwa ni matokeo ya amani na utulivu tulionao na usimamizi mzuri wa uchumi na sera nzuri za biashara na uwekezaji,”.

Serikali inaendelea kusimamia uletaji wa maendeleo ya nchi na watu wake kupitia miradi mikubwa ya kimkakati. “Katika kufanya hivyo tuna miradi mikubwa ya kimkakati ambayo nayo inakwenda hatua za mwisho isipokuwa mradi mmoja wa reli ambao kazi inaendelea,” alibainisha Rais Samia.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, mkoa wa Katavi umepokea karibu shilingi trilioni 1.2 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kukuza uchumi, kuimarisha maisha, na ustawi wa jamii pamoja na kusimamia utawala bora. Serikali imefanya maboresho makubwa katika huduma za afya ambapo changamoto ya upatikanaji wa dawa imepatiwa suluhisho. “Masuala ya madawa sasa hivi sio tena changamoto ukienda hospitali ukimuona daktari madawa yanapatikana,” alieleza Rais Samia.

Katavi pia imenufaika na shilingi milioni 37.2 kwa ajili ya ujenzi, ukarabati, na ununuzi wa vifaa tiba. Idadi ya magari ya kubeba wagonjwa imeongezeka kutoka 10 hadi 16, vituo vya huduma ya dharura kutoka 8 hadi 14, na watumishi wa afya kutoka 893 hadi 1,492. Katika sekta ya elimu, Katavi imepokea shilingi bilioni 7.9 kwa ajili ya shule za sekondari na shilingi bilioni 5 kwa ajili ya shule za msingi.

Rais Samia aliwashukuru wakulima wa Katavi na Tanzania kwa ujumla kwa juhudi zao na kuhakikisha kuwa serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na kujenga miundombinu ya umwagiliaji maji. Mkoa wa Katavi sasa una skimu 29 za umwagiliaji ambazo zimeongeza tija ya uzalishaji wa mpunga kutoka tani 1.5 kwa hekta mwaka 2007 hadi tani 4 kwa hekta mwaka 2024. Serikali inajipanga kuongeza skimu nyingine sita ndani ya mkoa huu.

Kwa kuongeza, juhudi zinaendelea ili kuhakikisha Katavi inaingia katika Gridi ya Taifa na hivyo kuwa na umeme wa uhakika. “Tunaendelea kufanya kila linalowekezekana ili Katavi nayo iingie katika Gridi ya Taifa na hivyo kuwa na umeme wa uhakika,” alisema Rais Samia.

Ziara ya Rais Samia mkoani Katavi imeonesha jinsi serikali inavyoweka juhudi kubwa katika kuhakikisha maendeleo na ustawi wa wananchi wake. Miradi ya afya, elimu, kilimo, na miundombinu inaendelea kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu wa Katavi na Tanzania kwa ujumla.

error: Content is protected !!