Dar es Salaam, Tanzania – Rais Samia Suluhu Hassan leo amewaapisha viongozi wapya katika sherehe iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam. Akihutubia wakati wa kuwaapisha viongozi hao, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa wizara ya habari katika utekelezaji wa falsafa ya serikali ya 4R, akionyesha nia thabiti ya kusimamia kikamilifu uhuru wa habari.
“Wizara ya habari ni muhimu sana katika utekelezaji wa ile falsafa yetu ya 4R, na hapa nitagusia uhuru wa habari kwamba lazima uendelee kusimamiwa kikamilifu,” alisema Rais Samia.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa sekta ya habari, Rais Samia alihimiza ushirikiano kati ya viongozi na wadau wa sekta hiyo. “Nenda kashirikiane na wadau wa sekta ya habari, watu wa sekta ya habari ni muhimu sana sana kwa taifa hili. Vyombo vyote vya habari ni muhimu sana kwa taifa letu,” aliongeza.
Katika mazungumzo yake, Rais Samia alilinganisha juhudi za kuunganisha miji na vijiji kwa barabara na umuhimu wa kuwaunganisha wananchi kupitia mawasiliano ya simu. “Kama tunavyojenga barabara kuunganisha miji na vijiji kwa kurahisisha mawasiliano hivyo hivyo, tunatakiwa kuwaunganisha wananchi na mawasiliano ya simu,” alisema.
Aidha, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kujenga uchumi wa kidigitali, akielekeza kwamba mifumo ya serikali inapaswa kuwa inasomana ifikapo Desemba mwaka huu. “Katika kujenga uchumi wa kidigitali, nilitoa maelekezo kwamba ifikapo Desemba mwaka huu mifumo ya serikali iwe inasomana. Taarifa inayopita sekta moja isomeke sekta nyingine kwa zile sekta zinazoingiliana,” alisema.