Dar es Salaam – Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kupokea The Gates Goalkeepers Award, tuzo inayotolewa na Bill & Melinda Gates Foundation, ikiwa ni heshima kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha sekta ya afya nchini.
Tuzo hiyo inamtambua Rais Samia kwa juhudi zake katika kupunguza vifo vya uzazi, kuimarisha huduma za afya kwa mama na mtoto, na kupanua upatikanaji wa huduma za afya kwa wote. Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Demografia na Afya ya mwaka 2022, vifo vya uzazi nchini vimepungua kwa asilimia 80, kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 hadi vifo 104 mwaka 2022.
Mbali na hilo, serikali yake imewekeza katika ujenzi wa hospitali na vituo vya afya, usambazaji wa vifaa tiba, na kuboresha upatikanaji wa bima ya afya kwa wananchi wengi zaidi. Uongozi wake pia umeimarisha huduma za chanjo na kupambana na magonjwa ya kuambukiza kama malaria na kifua kikuu.
Rais Samia anakuwa kiongozi wa kwanza wa Tanzania kupokea tuzo hii, ambayo hutolewa kwa watu wanaoleta mabadiliko makubwa katika maendeleo ya jamii na afya duniani.