Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo za ‘Samia Kalamu’ zitakazofanyika Aprili 29, 2025, jijini Dodoma. Tuzo hizo zimetolewa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa ushirikiano na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dk. Rose Reuben, na Mkurugenzi Mtendaji wa TCRA, Dk. Jabiri Bakari, tuzo hizo zinalenga kuhamasisha uandishi wa habari za maendeleo zenye uchambuzi wa kina, weledi, uzalendo, na maadili ya taaluma.
Tuzo hizo ni matokeo ya mafunzo ya uandishi wa habari za maendeleo yaliyotolewa mwaka jana, zikilenga waandishi wa habari, wachapishaji wa maudhui mtandaoni, maofisa habari, na watangazaji waliowasilisha kazi bora kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Zitahusisha vipengele mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tuzo ya Mwanahabari Mahiri Kitaifa, Tuzo za Uandishi wa Nishati Safi ya Kupikia, pamoja na tuzo maalum za kisekta katika maeneo ya afya, elimu, mazingira, utalii, kilimo, teknolojia, na mengine mengi.
Tuzo hizi ni sehemu ya juhudi za kuinua hadhi ya tasnia ya habari nchini, huku zikitambua mchango wa wanahabari katika kuleta maendeleo chanya kwa jamii.