Kufikisha miaka 30 ni kipindi cha mabadiliko makubwa kwenye maisha ya mtu na taaluma yake. Ni kipindi ambacho malengo ya wengi kitaaluma na familia huanza kuwa wazi na shauku ya kufika sehemu fulani kimaendeleo huongezeka zaidi.
Vijana wengi hasa wa kiume huwaza kutoka nyumbani na kuanza maisha yao binafsi ili kujiandaa kujenga familia. Kwa lugha nyingine ni muda wa kuachana na mambo ya kitoto na kuingia katika majukumu ya mtu mzima.
Katika mazingira kama hayo unatakiwa kufanya nini ili kufanikisha safari yako ya mafanikio?
Jifunze kutoka kwa wenzako
Kadri unavyozidi kukua katika taaluma yako kabla hajafika miaka 30 unatakiwa kujifunza siyo tu kwa wale waliokuzidi, bali hata kutoka kwa wale tulionao kwenye ngazi moja.
Hii itakuhakikishia ujenzi wa msingi wa maisha kwa sababu utapata mbinu nyingi za kuzikabili changamoto zinazoweza kuibuka wakati ukitekeleza mipango yako. Wao watakufunza uzoefu walionao katika maisha ambao unaweza kuwa msaada kwako.
Nidhamu katika matumizi ya pesa
Kuwa na nidhamu katika matumizi yako ya fedha, weka bajeti na hakikisha unaifuata. Acha kutumia pesa bila mipango.
Weka akiba ya kila pesa unayoipata. Jifunze kuweka akiba na utoke nyumbani kwenda kujitegemea mwenyewe. Hakikisha unalipa madeni yote unayodaiwa mapema mara upatapo pesa ili kuzuia yasikuandame kiasi cha kushindwa kulipika na achana na hisia kuwa kuna watu unawajibika kwao.
Fanya biashara na uwekezaji wa miradi
Kama hutaki kuajiriwa lakini unataka kufanya biashara, jitahidi uanze kuifanya kabla hujaoa au kuolewa. Utakuwa muoga sana na hutakuwa na uthubutu wa kutosha pale tu utakapoanza kuwa na familia na maendeleo ni ya muhimu kuanzia mwanzo wa taaluma yako.
Jenga tabia njema na maadili mazuri
Tabia inajengwa kuanzia kwenye matumizi mazuri ya muda, maadili ya kazi, kujiwekea mipaka ya kazi au maisha, mazoezi, kula vizuri au kuwa na nidhamu na fedha zako binafsi. Maadili ndiyo msingi wako mkuu wa kufanikisha maisha. Pale unapokutana na mazingira yasiyotabirika kwenye maisha, maadili mazuri uliyojijengea kwa muda mrefu ndiyo yatakayokusaidia.
Tunza mawasiliano
Jitahidi kutunza mawasiliano ya watu muhimu unaokutana nao katika shughuli mbalimbali za kikazi au biashara. Fanya vyovyote inavyowezekana ili kutunza mawasiliano yako siku zote. Mawasiliano ni muhimu maana hujui ni wakati gani utahitaji msaada kutoka kwa mtu fulani.
Fanya unachokipenda
Kila kijana ana kusudi lake la kuishi duniani. Tambua kile unachokipenda na lenga kuwa bora duniani katika kile unachokifanya kwa kupenda kujifunza zaidi kwa nadharia na vitendo.
Tafuta mwalimu au mtu ambaye amewahi kupita kwenye njia unayotamani kupita. Kuwa mbunifu, mwaminifu na heshimu muda unaoutumia pamoja naye kwasababu anajifunza kutoka kwako pia.
Tembelea maeneo mbalimbali
Hakuna kitu kizuri kinachofungua macho kama kusafiri kwenda sehemu mbalimbali ili kupanua uelewa wako na kuboresha mbinu zako za mawasiliano kutoka kwa watu wengine wa tamaduni tofauti. Hii inawezekana hata kama mfuko wako bado ni mdogo. Unachokipata hicho kitumie kufika hata maeneo ya karibu ujifunze mapya.
Uzoefu wa kidunia hauna gharama. Inakusaidia kufahamu mambo chanya kwenye ulimwengu halisi wa watu. Kuna watu wapo Dar es Salaam miaka 10 sasa hawajawahi kufika hata Bagamoyo au Mkuranga ambako kuna maisha tofauti na anapoishi kwa sasa.
Hata hivyo, wewe bado ni kijana mwenye nguvu nyingi, mwenye ushawishi na una muda mwingi wa kufanikiwa zaidi hata pale unaposhindwa unaweza kuanza tena na kufanikiwa maana huna cha kupoteza.