Waziri wa Mambo ya Nje Tanzania aanza ziara ya kikazi nchini China

HomeKimataifa

Waziri wa Mambo ya Nje Tanzania aanza ziara ya kikazi nchini China

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), amewasili jijini Beijing, China tarehe 9 Juni 2025 kwa ziara rasmi ya kikazi.

Akipokelewa na Bw. Xu Zhongsheng, kiongozi mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Watu wa China, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Khamis Mussa Omar, Mhe. Kombo atakuwa akiongoza ujumbe wa Tanzania katika mikutano na maonesho mbalimbali muhimu ya ushirikiano kati ya Tanzania na China.

Akiwa nchini humo, Waziri Kombo ataongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Uratibu wa Maazimio ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC), utakaofanyika kuanzia tarehe 11 hadi 12 Juni 2025. Aidha, atahudhuria Maonesho ya Nne ya Biashara ya Kimataifa kati ya China na Afrika yatakayofanyika mjini Changsha kuanzia tarehe 13 hadi 15 Juni 2025.

Katika ratiba yake, Waziri Kombo anatarajiwa pia kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Mhe. Wang Yi, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CCP). Mazungumzo hayo yanalenga kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na China.

Vilevile, Waziri Kombo na ujumbe wake watatembelea mikoa ya Sichuan na Shenzhen, ambako watakutana na viongozi wa maeneo hayo pamoja na wawakilishi wa kampuni kubwa za biashara na uwekezaji. Lengo ni kuhamasisha ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi, na kuvutia wawekezaji kutoka China kuja kuwekeza Tanzania.

Waziri huyo pia atatembelea Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Tanzania iliyopo mjini Guangzhou na kukutana na Watanzania wanaoishi katika jiji hilo.

error: Content is protected !!