SERIKALI imetoa Sh bilioni 69 kwa awamu ya kwanza katika kuhakikisha Wizara ya Mifugo inaendesha kampeni ya kutoa chanjo na kutambua mifugo yote iliyoko Tanzania kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ashatu Kijaji akizungumza na waandishi wa habari amesema zoezi la utambuzi wa mifugo na chanjo utafanyika kwa kipindi cha miaka mitano 2025 hadi 2029 hivyo zoezi la kuchanja mifugo na kutambua takwimu ya mifugo litafanyika kila mwaka kwa miaka mitano mfululizo.
Amesema kuwa zoezi hilo litafanyika kidigitali ambapo serikali imetoa vishikwanbi zaidi ya 4,000 pamoja na usafiri wa pikipiki kwa maofisa ugani 700 nchini na mafuta ambao watatoa huduma kwa kila kaya na kufikia kila mfugaji bure.
Amesema kwa awamu ya kwanza Ng’ombe milioni 19.7 watatambuliwa, kondoo milioni 17, mbuzi wa asili milioni 18 na kuku milioni 40 watafikiwa na kuchanjwa kwa lengo la kuwakinga na magonjwa nyemelezi.
Akizungumzia faida za chanjo amesema kuwa ni kutambua mahitaji ya mifugo, uwezo wa kutoa huduma, uwezo wa kutoa ajira, urahisishaji wa huduma za ugani utafiti na mafunzo kwa wafugaji nchini, pamoja na kudhibiti vitendo vya wizi.
Ametoa wito kwa maofisa wa serikali watakaoshiriki zoezi hilo kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa wafugaji na kukamilisha zoezi hilo kwa muda uliopangwa ambapo gharama zote zimegharamiwa na serikali.