Ziara ya siku saba (Juni 15 – Juni 21, 2025) ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika mikoa ya Simiyu na Mwanza imebadili maisha ya wananchi wa mikoa hiyo kwa kuyafanya kuwa bora zaidi kutokana na miradi iliyozinduliwa. Miradi hiyo itachochea usalama wa wananchi, kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii na kukuza uchumi wao, ikiwa ni alama ambayo hawatoisahau.
Akiwa mkoani Simiyu Mheshimiwa Rais alifungua viwanda vitatu vya kuchakata/kuchambua pamba ambavyo vinatoa ajira, kuongeza tija ya zao la Pamba na kukuza sekta funganishi. Aidha, alifungua Shule ya Wasichana ya Sayansi Simiyu, shule ya amani, majengo ya utawala, mradi wa maji, hospitali pamoja na kampeni ya chanjo na utambuzi wa mifugo, miradi ambayo ni utekelezaji wa ahadi ya serikali ya kuboresha maisha ya wananchi.
Baada ya kuhitimiza ziara mkoani Simiyu, alikwenda Mwanza ambapo aliandika historia kwa taifa letu kwa kufungua Daraja la JP Magufuli ambalo litabadili kwa kila namna maisha ya wakazi wa Kanda ya Ziwa. Daraja hilo ambalo ni ndoto ya miaka mingi ya wananchi, litapunguza muda wa kuvuka katika Kigogo na Busisi toka zaidi ya saa moja, hadi dakika nne kwa gari, hivyo kuchochea ukuaji wa biashara kwa mikoa hiyo na nchi jirani pia ni alama ya utambulisho na uhuru wa taifa letu.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Rais amezindua Mradi wa Maji wa Butimba ambao utamaliza kero ya maji kwa wananchi 450,000. Kama hilo halitoshi, tayari boti ya uokozi katia Ziwa Victoria iko njiani ikipelekwa mkoani Mwanza ili kuimarisha usalama wa watumiaji wa ziwa hilo wanaolitegemea kuendesha maisha yao.
Makubwa haya ambayo yamefanyika katika mikoa hiyo ni sehemu ya makubwa mengi yaliyofanyika kwenye mikoa mingine ndani ya miaka mnne. Kutokana na hayo, katika kila mkutano aliozungumza, wananchi wamemwahidi kwamba watampa kura ya NDIYO ili aendeleze miradi inayowanufaisha.