Mradi wa Maji Nangano kunufaisha wakazi 1,428

HomeKitaifa

Mradi wa Maji Nangano kunufaisha wakazi 1,428

Zaidi ya wakazi 1,428 wa Kijiji cha Nangano, Wilaya ya Liwale mkoani Lindi wameanza kunufaika na mradi wa maji ya bomba uliomaliza adha ya kutembea zaidi ya kilometa tatu kwenda kuchota maji katika Mto Mbwemkuru.

Mradi umegharimu kiasi cha shilingi 461,448,579 ambapo shilingi 455,448,579 kutoka Serikali kuu na shilingi 6,000,000 kutoka kwa wananchi.

Utekelezaji wa mradi wa maji Nangano umehusisha ujenzi wa tangi la kuhifadhi maji lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 50,000 na ujenzi wa vituo vitano vya kuchotea maji.

Mkazi wa Kijiji cha Nangano, Rehema Mkwepu aliishukuru serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao umemaliza mateso ya muda mrefu kutumia maji ya mito na visima pamoja na wanyama wa porini wakiwemo nguruwe na tembo.

“Tangu Uhuru wa Tanganyika na sasa Tanzania mwaka 1961 hatukuwahi kupata mradi wa maji wa bomba katika kijiji chetu, badala yake maji ya bomba tulitumia pindi tunapokwenda makao makuu ya Wilaya ya Liwale mjini au Hospitali ya Wilaya hivyo mradi huo umeleta fraja kubwa kwetu.

Lengo la kujenga mradi huo ni kusogeza huduma ya majisafi na salama karibu na wananchi wa kijiji hicho katika umbali usiozidi meta 400 na kuboresha afya za wananchi ambao awali walilazimika kutumia maji ya visima na mito ambayo maji yake hayakuwa safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

error: Content is protected !!