Makampuni 16 ya Kitanzania yameidhinishwa rasmi na Mamlaka ya Forodha ya China — General Administration of Customs of China (GACC) — kusafirisha parachichi kwenda katika soko la China. Taarifa hii imetolewa na Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, ambaye amesema hatua hiyo ni sehemu ya uhusiano mzuri na wa kimaendeleo kati ya mataifa haya mawili.
Uamuzi huo ni mafanikio makubwa kwa Tanzania na unatokana na juhudi za kidiplomasia zilizoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Tangu aingie madarakani, Rais Samia ameweka msukumo mkubwa katika kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa lengo la kufungua masoko ya nje kwa bidhaa za wakulima wa Tanzania.
Makampuni hayo 16 yamepitia mchakato wa uhakiki wa viwango vya ubora na usalama wa chakula unaoendana na masharti ya soko la China. Hatua hii inaiweka Tanzania kwenye nafasi nzuri ya kushindana kimataifa katika sekta ya mazao ya kilimo, hususan parachichi, ambayo imeendelea kupata umaarufu duniani.
Kupatikana kwa soko la China kunatarajiwa kuleta ongezeko la mapato kwa wakulima wa Kitanzania, kuongeza ajira, na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kilimo vijijini. Aidha, hatua hiyo inaimarisha nafasi ya Tanzania kama mzalishaji mahiri wa mazao bora ya kilimo katika bara la Afrika.
Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima kupitia maboresho ya miundombinu, elimu ya kilimo bora, na utafutaji wa masoko ya nje. Uamuzi wa China kufungua rasmi milango yake kwa parachichi za Tanzania ni ushahidi wa mafanikio ya mikakati hiyo ya serikali.
Kwa mujibu wa Balozi wa China nchini Tanzania, uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa haya mawili utaendelea kuimarika, huku China ikisisitiza kuwa itaendelea kufungua milango yake kwa dunia kwa ajili ya maendeleo ya pamoja.