Bingwa kuingiza watalii Tanzania

HomeKimataifa

Bingwa kuingiza watalii Tanzania

Idadi ya watalii waliotembelea Tanzania miezi mitano iliyopita imeongezeka hadi kufikia 458,048 huku nchi ya Kenya ikiwa ni miongoni mwa nchi zilizoingiza watalii wengi. 

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika taarifa yake iliyotolewa hivi karibuni kuhusu watalii walioingia Tanzania kati ya Januari na Mei, 2022 imeeleza kuwa idadi hiyo ya watalii imeongezeka kutoka 317,270 waliotembelea nchini kipindi kama hicho mwaka jana.

“Hilo ni ongezeko la watalii 140,778 sawa na asilimia 44.3,” imeeleza NBS katika taarifa hiyo ambapo watalii wote walitoka katika mataifa 211 duniani.

Watalii waliotembelea Tanzania miezi mitano ya mwanzo ya 2022 kwa sehemu kubwa walitokana katika nchi tano duniani za Kenya, Burundi, Ufaransa, Poland na Marekani ambapo ziliingiza watalii 165,985 sawa na asilimia 36.2 ya watalii wote walioingia nchini katika kipindi hicho.

Kwa mujibu wa  NBS, Kenya ndiyo imeongoza kuingiza watalii wengi ambapo jumla ya watalii 55,388 ikifuatiwa na Burundi (38,170) na  Ufaransa katika nafasi ya tatu ambapo iliingiza watalii 28,115.

Poland imeshika nafsi ya nne kwa kuingiza watalii 22,651 huku Poland ikifunga tano bora kwa watalii 21,661.

Februari ndiyo mwezi ambao Tanzania ilipokea watalii wengi zaidi katika kipindi hicho cha miezi mitano  iliyopita ambapo walikuwa 101,042 huku Aprili waliingia watalii wachache zaidi wanaofikia 79,405.

Sababu za kuongezeka watalii

Fredy Mushi, muongoza watalii kutoka kampuni ya Kilele Climb Tours anasema watalii wengi wanavutiwa na hali ya ukarimu ya Watanzania na mapokezi mazuri wanayoyapata.

“Watalii wengi hasa kutoka Marekani wanavutiwa na hali ya ukarimu wa Watanzania na mapokezi ambayo watu wa  nchi hii huwaonyesha wageni” anasema Mushi.

Mushi anasema kuongezeka kwa watalii pia kunaweza kuchangiwa na mazingira rafiki ikiwemo vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania.

Huenda idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania ikaongezeka zaidi mwaka huu baada ya kuzinduliwa kwa filamu ya “Royal Tour” ambayo inaonyesha vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Mwaka jana Tanzania ilipokea watalii 922,692 kutoka watalii 620,867 wa mwaka 2020. Ujio wa watalii uliathiriwa na ugonjwa Corona (Uviko-19). 

Shabaha ya Tanzania ni kufikisha watalii milioni 5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2030.

 

error: Content is protected !!