Ufafanuzi kuhusu tozo

HomeKitaifa

Ufafanuzi kuhusu tozo

Hatimaye baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wananchi kuhusiana na tozo za miamala ya simu zilizoanza kutozwa na Serikali Julai Mosi mwaka huu, Serikali imeahidi kuyafanyia kazi siku chache zijazo.

Waziri wa Fedha na Mipango Dk Mwigulu Nchemba aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Septemba Mosi kuhusu tozo kwenye miamala ya simu na benki amesema wameyapokea maoni yaliyotolewa na wananchi na wanayafanyia kazi.

“Tumepokea, yameshafika serikalini, tutachambua na kuweka utaratibu wa utekelezaji wake siku, siyo nyingi tutakuja na majibu ya namna ya kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa,” amesema Dk Mwigulu.

Itakumbukwa miongoni mwa yanayolalamikiwa kuhusu tozo ni mtu kukatwa mara mbili kutoka  benki na kwenye simu pamoja na mkanganyiko wa ulipaji wa kodi ya pango kwa nyumba binafsi ambapo amesema hoja hizo zina mantiki na wanapokea maoni ili kurekebisha.

Hata hivyo Waziri Mwigulu amesema chimbuko la tozo ya miamala ya benki ni  kupunguzwa kwa viwango vya tozo kwenye miamala ya simu ambapo waliona ni vema kuongeza wigo wa ukusanyaji mapato.

Aidha, amesema kuwa tozo siyo kodi ya kibiashara bali ni ushirikiano wa pamoja wenye  lengo la  kuongeza nguvu ya kutimiza mambo ya lazima ambayo hayapo kwenye bajeti.

“Chimbuko la tozo ni kwa ajili ya kuunganisha nguvu kama Watanzania ili kutekeleza baadhi ya mahitaji ya lazima ambayo yamekuwa yakikosa bajeti kutokana na ufinyu wake kama madarasa, nyumba za walimu, vituo vya afya na vifaa tiba na miundombinu” amesema Mwigulu.

Ufinyu wa bajeti umetokana kuongezeka kwa mahitaji ikiwemo ujenzi wa miradi mikubwa kama bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo kwa mujibu wa Nchemba miradi hiyo inakadiriwa itatumia Sh29 trilioni.

Amesema serikali itaendelea kupanua wigo wa ukusanyaji wa kodi kwa kila mtu mwenye mapato na anayestahili kulipa pamoja na kuongeza vyanzo vipya vya tozo jambo litakalosaidia kupunguza kiwango cha tozo.

Kwa mujibu wa waziri huyo, tozo ni pendekezo la wananchi na inalenga kuboresha huduma za kijamii ambazo zinamfaidisha kila mtu.

Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amesema tangu kuanzishwa kwa tozo ya miamala ya simu na benki,  Serikali imefanikiwa kutekeleza miradi kadhaa katika nyanja za elimu, afya na miundombinu,  jambo ambalo lisingefanikiwa bila tozo.

Bashungwa amesema kupitia tozo Serikali imejenga jumla ya vituo vya afya 234 kwa Sh117 bilioni, pamoja na kununua vifaa tiba vyenye thamani ya Sh149.5 bilioni.

Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu amesema kupitia tozo Serikali imefanikiwa kulipa malimbikizo ya mishahara pamoja na kuwapandisha madaraja wafanyakazi.

“Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Februali 2022 Serikali ililipa malimbikizi ya mishahara wa watumishi 55,235 yenye thamani ya Sh93. 3 bilioni na katika kipindi Cha Machi-June 2022 watumishi wengine 17,530 walilipwa malimbikizi ya mshahara yenye thamani ya Sh58.7 bilioni,” amesema Prof Ndalichako.

error: Content is protected !!