Wakala ya Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) umesema kuwa tangu kuanzishwa kwake, wamefanikiwa kujenga jumla ya madaraja 439 ya mawe yenye thamani ya Sh bilioni 15, hatua ambayo imewezesha kuokoa kiasi kikubwa cha fedha.
Hayo yamebainishwa na Mhandisi Mshauri wa TARURA, Pharles Ngeleja, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Ngeleja ameleza kuwa, ujenzi wa madaraja ya mawe unatoa nafuu kubwa ya gharama, na unazingatia mabadiliko ya hali ya hewa ambayo huathiri miundombinu mingine.
”TARURA tumeona umuhimu wa kutumia teknolojia ya madaraja ya mawe, ambayo ni nafuu na inaendana na mazingira ya vijijini.
“Kwa madaraja haya 439, tumetumia Sh bilioni 15. Ikiwa tungetumia njia ya ujenzi wa madaraja ya zege, tungeweza kutumia zaidi ya Sh bilioni 90. Hivyo, ujenzi wa madaraja ya mawe umewezesha kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za serikali,” amesema Ngeleja.
Ngeleja amezungumzia umuhimu wa miundombinu ya barabara katika kusaidia maendeleo ya kilimo akisisitiza kwamba, kupitia ujenzi wa miundombinu bora, wakulima wanaweza kufikia masoko kwa urahisi, jambo ambalo linachangia katika kuongeza kipato na kuboresha uchumi wa maeneo ya vijijini.
”Kama mnavyojua, TARURA ndiyo mshipa wa damu wa wakulima. TARURA inawawezesha wakulima kufika kwenye masoko kwa urahisi. Hata kama mkulima alime kwa kiasi kikubwa, kama hana barabara, hawezi kufikia malengo yake. Hivyo, miundombinu bora ya barabara ni muhimu katika kuleta maendeleo ya kilimo na kuongeza uzalishaji,” ameongeza.
Katika maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, TARURA imekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu na kuonyesha mafanikio yake katika kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja, jambo ambalo linasaidia kuboresha maisha ya wananchi na kuongeza fursa za maendeleo katika maeneo ya vijijini.