Wakulima 368 mkoani Mara kunufaika na zana za umwagiliaji wa kisasa

HomeKitaifa

Wakulima 368 mkoani Mara kunufaika na zana za umwagiliaji wa kisasa

Wakulima wadogo 368 kutoka mkoa wa Mara wamepata neema baada ya kukabidhiwa jozi 34 za mashine za umwagiliaji zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 400. Vifaa hivyo vimetolewa kama sehemu ya juhudi za serikali kuboresha kilimo cha umwagiliaji na kuongeza uzalishaji wa mazao ya bustani na mbogamboga.

Makabidhiano ya vifaa hivyo yamefanyika mkoani Mara, yakihusisha kata 15 zilizoko katika Manispaa ya Musoma, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma, na Halmashauri ya Wilaya ya Rorya. Mradi huo unalenga kuwawezesha wakulima wadogo kutumia teknolojia ya kisasa ya umwagiliaji ili kuongeza tija, kupunguza utegemezi wa mvua, na kuhakikisha uzalishaji wa mazao kwa mwaka mzima.

Baadhi ya wakulima walionufaika na mpango huo wameishukuru serikali kwa kuwapatia msaada huo, wakisema utaleta mabadiliko makubwa katika maisha yao wakibainisha kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemea mvua katika kilimo, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto wakati wa vipindi vya ukame. Kupitia vifaa hivi vya umwagiliaji, sasa watakuwa na uhakika wa mavuno na soko la mazao yao kwa mwaka mzima.

Ugawaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya juhudi endelevu za serikali za kuendeleza kilimo cha kisasa na cha umwagiliaji, kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa na kilimo chenye tija, cha kibiashara, na chenye mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

error: Content is protected !!