Rais Samia ataka viongozi wasimamie fedha za miradi ya maendeleo

HomeKitaifa

Rais Samia ataka viongozi wasimamie fedha za miradi ya maendeleo

Rais Samia amewataka viongozi na watendaji wahakikishe wanasimamia matumizi sahihi ya fedha zinazoelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Rais Samia ameyasema hayo kwenye hafla ya Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere na Wiki ya Vijana iliyofanyika katika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera jana (14, Oktoba 2022).

“Tunafanya hivyo tukiamini viongozi na watendaji wa ngazi zote watahakikisha wanasimamia matumizi sahihi ya fedha zinazopelekwa kwao kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” ameongea Rais Samia.

Rais Samia pia amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wasiojali na kuhurumia wananchi kwa kuwapa miradi wakandarasi wasio na uwezo na kusababisha miradi kutotekelezwa ipasavyo.

“Inasikitisha kuona kwamba kuna watu wasiojali na wasio na huruma kwa wananchi kwa  kuwapa miradi wakandarasi wasio na uwezo, watu waliotawaliwa na rushwa, wezi na wengine ni wazembe wanaosababisha miradi kutokukamilika,” amesema Rais Samia

Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2022 zilikuwa na ujumbe maalumu wa sensa chini ya kauli mbiu isemayo ‘Sensa ni Msingi wa Maendeleo Shiriki Kuhesabiwa Tuyafikie Maendeleo ya Taifa’.

Mbio hizo zilizinduliwa Aprili 2, 2022 ambapo miradi ya maendeleo 1,293 iliyogharimu Sh6508 bilioni ilizinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi katika maeneo mbalimbali hapa nchini

error: Content is protected !!