Wananchi wasilisheni taarifa za vurugu za Oktoba 29

HomeKitaifa

Wananchi wasilisheni taarifa za vurugu za Oktoba 29

Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani uliotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imeanza rasmi kazi zake.

Tume hiyo chini ya uenyekiti wa Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande Othman, imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Novemba 19, mwaka huu ikiwa na wajumbe wengine saba ambao ni Watanzania wabobezi katika masuala mbalimbali.

Majukumu ya tume hiyo ni pamoja na kuchunguza chanzo cha machafuko ya Oktoba 29, mwaka huu, kuwabaini waliohusika, kutathmini madhara yaliyojitokeza na kupendekeza hatua za kuimarisha amani, usalama na umoja wa kitaifa.

Katika taarifa yake kwa umma, tume imewaita wananchi watoe taarifa, ushahidi, maoni na mapendekezo yatakayosaidia katika uchunguzi wake. Kwa mujibu wa Jaji Mkuu mstaafu Chande, mafanikio ya kazi hiyo yatategemea ushirikiano wa wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia kubainisha ukweli.

Tungependa kusisitiza umuhimu wa Watanzania wenye taarifa kama ambavyo tume imeeleza, kujitokeza na kuziwasilisha kwao ili kusaidia katika kuhakikisha tume inakuja na majawabu ya nini hasa kilichotokea Oktoba 29, mwaka huu.

error: Content is protected !!