Ujenzi wa kituo cha mafunzo ya Uongezaji thamani madini waanza

HomeKitaifa

Ujenzi wa kituo cha mafunzo ya Uongezaji thamani madini waanza

Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kukamilisha ujenzi wa majengo ya kituo cha mafunzo ya Uongezaji thamani madini ya vito kwa kuongeza nguvukazi na kufanya kazi kwa masaa 24 ili kukamilisha ujenzi wa jengo kwa muda mfupi.

Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Desemba 12, 2025 mkoani Arusha wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa kituo hicho ulioanza ujenzi rasmi ambapo katika maelekezo yake amemtaka mkandarasi kuzingatia ujenzi bora wenye kukidhi vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais.Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza mikakati yake kwenye mnyororo mzima wa uongezaji thamani madini ya vito kama Sera ya Madini ya Mwaka 2009 inavyoelekeza.

Sambamba na hapo, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, kuanza kwa ujenzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia Bunge la 13 jijini Dodoma.

Waziri Mavunde amebainisha kuwa, kukamilika kwa kituo hicho , kutaleta faida mbalimbali ikiwa pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watakao jiunga kwenye kituo, kuongezeka kwa wataalamu wa uongezaji thamani madini ya vito, kufungua fursa za ajira kwa vijana na wafanyabiashara wa madini , pamoja na kutosafirishwa kwa madini ghafi nje ya nchi hivyo kutachagiza ongezeko la mapato kwa taifa.

Kwa upande wake , Mkuu wa Wilaya Arusha Mhe. Joseph Mkude ameahidi kuendelea kufuatilia maendeleo ya ujenzi ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kama Serikali inavyotaka.

Kitakavyokuwa kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) baada ya kukamilika

error: Content is protected !!