Haya ni mambo 10 muhimu ya kuzingatia ili kupunguza/kubana matumizi ya mafuta kwenye gari yako.
1. Endesha tu pale kwenye tija
Kuwa na sababu ya kuendesha gari yako, ifanye gari yako iwe na kazi maalumu kama kuendea kazini au kupeleka watoto shule. Kuna sehemu nyingine ambazo ziko karibu tu sio lazima uwashe gari, changamsha miguu au tafuta baiskeli. Sawa gari ni yako, ila kuiendesha bila sababu za msingi na kipato chako kama sio kikubwa, itakugharimu mwisho wa siku uone gari ni tatizo kumbe tatizo ni wewe.
2. Hakikisha kifuniko cha tenki kimekaza vizuri
Inawezekana unakumbana na tatizo la mafuta kuisha haraka kwenye gari yako na pengine usijue tatizo. Mafuta yanaweza kukauka kupitia njia ya mvuke (Evaporation) kama ikiwa kifuniko hakijakazwa vizuri.
3. Usiache gari lako lina unguruma bila sababu
Kuacha gari linaunguruma kwa muda mrefu ni moja ya sababu zinazokula kwa kasi mafuta ya gari yako. Kuna sehemu huna budi kusimama wakati bado gari linawaka, kama vile kusubiri taa za barabarani. Lakini kama umewasili sehemu ya karibu, ni vyema ukazima gari yako kupunguza ulaji wa mafuta.
4. Vuta mafuta kiasi ukiendesha
Wakati unaendesha gari, usigandamize sana mguu kuvuta mafuta, kanyaga kiasi kwani kukanyaga sana mafuta hutumia mafuta mengi zaidi ya kawaida.
5. Endesha spidi/mwendo wa kawaida
Hakika kila gari lina kiwango fulani cha spidi kilichowekwa. Ukiendesha gari mbio zaidi ndio mafuta kwenye gari yako yatalika zaidi. Kama uko sehemu ambazo ni highway, ambazo zinakutaka uendeshe gari kwa kasi ni sawa, lakini sio lazima kuendesha mwendo mkubwa katika mazingira yako ya kila siku kama unataka kubana matumizi ya mafuta. Lakini hili hutegemea pia ukubwa wa njia ya gari lako.
6. Usikanyage mafuta kwenye mteremko
Unapokuwa kwenye mteremko usikanyege mafuta , hii inasaidia kubana matumizi ya mafuta. Gari lako linashuka kwenye mteremko kutokana na gravity/ mteremko, katika mazingira haya injini hufanya kazi lakini haili mafuta.
7. Punguza matumizi ya kiyoyozi (AC)
Kwa mazingira kama ya Dar es Salaam ambapo joto ni kubwa wakati mwingine, matumizi ya AC ni muhimu sana. Lakini sio kila wakati ni lazima uwashe AC, unaweza kuizima ukafungua kioo kidogo kuruhusu hewa kuingia na kutoka ndani. Matumizi makubwa yasiyo ya lazima ya AC huenda sambamba na matumizi makubwa ya mafuta.
8. Hakikisha unasafisha vichuja hewa (Air Filters) mara kwa mara
Chujio hizi maalumu zinapaswa kuwa safi ili ifanye kazi vizuri na kurahisishia kazi ya injini ya gari lako. Air filter zinapokuwa chafu husababisha injini kufanya kazi zaidi ya ambavyo inatarajiwa kufanya hivyo hupelekea ulaji mkubwa zaidi wa mafuta. Kila gari ina taratibu zake za kusafisha Air Filters, hakikisha unafuata utaratibu wa gari lako.
9. Hakikisha tairi zako zina ujazo wa hewa inaotakiwa
Hakika tairi zako zote zina ujazo sahihi wa upepo. Upepo pungufu kwenye tairi hupelekea matumizi makubwa ya mafuta. Gari ikiwa na upepo kidogo inakuwa nzito na uzito wa gari huongeza kazi kubwa kwenye engine na hatimaye ulaji wa mafuta nao unaongezeka.
10. Punguza uzito wa gari yako
Kuna watu wengine wana hulka ya kupenda kuongeza vitu ambavyo havina msingi kwenye magari yao hivyo kuongeza uzito kwenye gari. Wataalamu wa magari wanasema kwa kila kilogram 45 inayoongezeka kwenye gari, uwezo wa kutunza mafuta wa gari yako unapungua kwa asilimia 2.
Mambo haya hayaishii hapa, yapo mengi zaidi. Kikubwa ni kuyafanya kwa usahihi ili gari lako lisitumie mafuta mengi.