Dereva alifariki kabla basi kupinduka

HomeKitaifa

Dereva alifariki kabla basi kupinduka

Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, George Kyando amesema dereva wa basi la Kampuni ya Zuberi, Hamza Haule, alifariki kabla ya basi hilo halijaanguka na kusababisha vifo na majeruhi.

Alisema kuwa kwa mujibu wa taarifa ambazo jeshi hilo lilizipata na inaendelea na uchunguzi ili kubaini ukweli, zinadai kuwa dereva huyo kabla ya kuanza safari kutoka Mwanza kwenda Kahama, hakuwa vizuri kiafya na alipofika eneo hillo la Mwigumbi, alifariki dunia akiwa kwenye usukani.

“Ajali hii imegharimu maisha ya watu watano, watu wawili wamefia hapo hapo kwenye eneo la tukio na watu watatu walifia hospitalini.

“Ninatoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto wawe wanachunguza afya zao kabla ya kuanza safari na endapo wakiwa hawajisikii vizuri, wasiendelee na safari ili kuepusha ajali zisizo za lazima,” alisema RPC Kyando.

Baadhi ya majeruhi wa ajali hiyo, akiwamo Daniel Sewe, walisema walipofika kwenye eneo hilo la Mwigumbi, basi lilipiga tuta na kuanza kuyumba kisha kupoteza uelekeo na kugonga kingo za daraja,likapaa juu na kuanguka.

Basi la Kampuni ya Zuberi lenye namba za usajili T435 DJS likiwa limepinduka

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Kolandoto, Dk. Masunga Maneno, alisema hadi sasa watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni watano- watu wazima wanne na mtoto mmoja na walipokea majeruhi 26. Kati yao 13 walitibiwa na kuruhusiwa.

error: Content is protected !!