Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, amewasilisha wito rasmi kwa Tanzania kufungua ubalozi wake Vatican, hatua itakayodumisha na kuimarisha mahusiano kati ya pande hizo mbili.
Wito wa Papa Leo, umeelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican, Askofu Mkuu, Paul Gallagher alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Hatua hiyo, itaifanya Tanzania kuwa na uwakilishi Vatican, badala ya sasa inapowakilishwa kutokea Ujerumani.
Hayo yameelezwa jana, Jumatano Januari 28, 2026 wakati wa ziara ya Balozi Kombo, Vatican alipokutana na Papa Leo kuwasilisha ujumbe wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Katika kikao hicho pia Papa ameahidi kuiombea Tanzania amani na utulivu, baada ya vurugu za Oktoba 29, mwaka jana, huku akidokeza amewahi kuishi nchini katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Ruvuma na Arusha.
Ahadi hiyo ya Papa Leo, imetokana na ombi lililowasilishwa kwake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo alipomtembelea Vatican, kuwasilisha ujumbe wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.




