Serikali imesema inaendelea na taratibu za kufungua soko la dengu nchini Malaysia.
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde ametoa kauli hiyo bungeni leo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Itigi, Yohana Msita aliyeuliza nini mpango wa serikali kupandisha bei ya zao la dengu baada ya bei kuporomoka.
“Upatikanaji wa soko hilo utaruhusu zao la dengu kuingia rasmi katika soko la Malaysia. Hatua hiyo itaongeza wigo wa masoko na hivyo kuimarisha bei kwa wakulima,” amesema.
Pia amesema serikali imeanza kutekeleza mkakati wa kusambaza mbegu bora za dengu nchini ambapo katika mwaka 2025/2026, wizara imepanga kusambaza kilo 400 za mbegu mama za dengu kwa wakulima wa Halmashauri ya Itigi zenye uwezo wa kuzalisha tani nne za mbegu bora.
“Lengo ni kuhakikisha wakulima wanaongeza tija na uzalishaji ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa na kuwawezesha wakulima kupata bei nzuri,” amesema.


