Zimbabwe yapendekeza kuongeza mihula ya Rais na Bunge hadi miaka saba

HomeKimataifa

Zimbabwe yapendekeza kuongeza mihula ya Rais na Bunge hadi miaka saba

Baraza la Mawaziri la Zimbabwe limeidhinisha muswada wa marekebisho ya Katiba unaolenga kuongeza muda wa mihula ya Rais na Bunge kutoka miaka mitano hadi saba, hatua ambayo inaweza kumuweka madarakani Rais Emmerson Mnangagwa hadi mwaka 2030 badala ya 2028.

Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Mawaziri, mabadiliko hayo yanalenga kuimarisha mwendelezo wa sera na kutoa fursa kwa utekelezaji wa mipango ya muda mrefu kukamilika ipasavyo.

Muswada huo pia unapendekeza marekebisho katika utaratibu wa kumchagua Rais pamoja na muundo wa vyombo vya usimamizi wa uchaguzi.

Pendekezo la kuongeza muda wa mihula ni sehemu ya mjadala mpana ambao umekuwa ukiendelea nchini Zimbabwe kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Hapo awali, Rais Mnangagwa amekanusha kuwa na nia ya kuongeza muda wake wa uongozi zaidi ya mihula miwili iliyoainishwa katika Katiba ya sasa, akijitaja kuwa ni muumini wa Katiba na kusisitiza kuwa atang’atuka mwaka 2028, pale muhula wake wa pili wa kuchaguliwa utakapokamilika.

Muswada huo sasa unaelekezwa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na kupitishwa.

error: Content is protected !!