Serikali ya Tanzania Jumamosi imezindua mradi wa kusambaza umeme wa jua unaolenga visiwa 120 vilivyopo katika mikoa minane inayopakana na maziwa makuu pamoja na Bahari ya Hindi.
Mradi huo unakusudia kufunga mifumo ya umeme wa jua wa majumbani 20,000 kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 8 za Kitanzania (sawa na takribani dola milioni 3.2 za Marekani).
Mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ulizinduliwa rasmi na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, katika Kisiwa cha Bezi kilichopo Ziwa Victoria, wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Mikoa mingine itakayonufaika na mpango huo ni Geita, Kagera na Mara inayozunguka Ziwa Victoria; Rukwa inayopakana na Ziwa Rukwa; pamoja na Lindi, Mtwara na Pwani inayopakana na Bahari ya Hindi.
Makamba alisema serikali itatoa ruzuku ya hadi asilimia 75 ya gharama za kuunganishiwa umeme ili kuhakikisha wananchi wa maeneo ya mbali wanapata huduma hiyo kwa gharama nafuu.
Aliongeza kuwa mradi huo utaunga mkono moja kwa moja ajenda ya uchumi wa buluu nchini kwa kuwawezesha wavuvi kuongeza thamani ya mazao ya samaki kabla ya kuyauza sokoni, pamoja na kukuza ufugaji wa samaki, kilimo cha mwani na utalii wa fukwe.


