Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kama moja ya vivutio vikubwa vya uwekezaji katika sekta ya madini baada ya kushika nafasi ya 34 kati ya maeneo 68 duniani katika Investment Attractiveness Index (IAI) ya mwaka 2025, kwa mujibu wa ripoti ya Fraser Institute.
Katika bara la Afrika, Tanzania imeorodheshwa katika nafasi ya nne nyuma ya Botswana, Morocco na Zambia, hali inayoonesha ushindani wake katika kuvutia mitaji ya kimataifa ya utafiti na uwekezaji wa madini.
Ripoti hiyo pia inaonesha kupanda kwa alama za Tanzania katika IAI hadi kufikia 68.04 mwaka 2025 kutoka 62.75 mwaka 2024 na 46.38 mwaka 2023, ishara ya kuongezeka kwa imani ya wawekezaji katika sekta ya madini nchini.
Wadau wa sekta ya uchumi na madini wamempongeza Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuimarisha mazingira ya uwekezaji, wakieleza kuwa sekta ya madini inaendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania.


