Ijue sayansi anayoitumia Rais Samia kwenye hotuba zake

HomeUncategorized

Ijue sayansi anayoitumia Rais Samia kwenye hotuba zake

Kuzungumza mbele ya hadhira ya kipawa, kipawa ambacho si kila mtu ametunukiwa. Walikuwepo wahutubi wengi mahiri ambao majina yao yamekozwa kwenye vitabu vya historia kutokana na uwezo wao mkubwa katika katika kutoa hotuba. Viongozi kama Julius Nyerere, Albulhamid Kishki, Martin Luther Jr na wengine lukuki ambao wanasifika kwenye sanaa hiyo.

Mwingine wa kizazi hiki ni Mama, Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anaonekana mwenye kipawa hiki adimu cha kuhutubu. Rais Samia anaoneka kujua kwenye kuiteka hadhira pindi azungumzapo, naam, kwani hutumia lugha yenye vionjo vyenye misamiati mipya kila uchwao. Rais Samia ni mzuri sana wa kutumia misemo, nasahu na methali kwenye hotuba zako. Hii yote ni kwenye kutia mkazo kwenye suala fulani au kufurahisha kadanamsi kwa minajili ya kuwatoa uchovu.

Sasa hebu tatazamie namna ambayo Rais Samia hutumia Sayansi katika hotuba zake nzuri na zisizochosha kusikiliza. Hapa ni si tu kwenye hotuba rasmi ambazo zimeandaliwa kwa muda, bali hata zile ambazo huzungumza na hadhara kwa ghafla.

  1. Kujitweza
    Kama ni mfuatiliaji wa hotuba za Rais Samia, basi ni wazi umeiona hali ya kujitweza/kujishusha/kujidogosha kutoka kwake. Rais Samia hutumia lugha kama “Ndugu zangu”, “nawaomba”, “tukafanya”, “tutafanya”, “twendeni” na mengine mengi yanayo akisi unyenyekevu wake. Rais Samia kutumia maneno hayo ni katika hali ya kujiweka daraja moja na watu wake, ni hali ya kuonesha kuwa taifa hili ni letu sote na kila mmoja ana wajibu. Hata akiwa anatoa amri, basi utamsikia akiomba jambo fulani lifanyike kana kwamba ni hiari. Katika kuweka mazingira mazuri ya wafanyakazi serikalini kutekeleza majukumu yao sawia, basi kwa kiongozi wa kaliba yake kujitweza kwa kiasi hicho, ni jambo aula sana katika utekelezaji ya majukumu ya kila siku.
  1. Methali na Misemo
    Rais Samia ameonekana kuwa hodar sana katika matumizi ya semi, tungo, methali pamoja na nahau katika hotuba zake. Hii inaweza kuchochewa na yeye kuwa na mahaba ya lugha yetu ya Kiswahili, na pia makuzi na malezi aliyoyapata kutoka Pwani ambako ndio asili yake. Ni aghalabu sana kukuta Rais Samia hajatumia msemo au methali katika hotuba zake, haijalishi itakuwa fupi kiasi gani, na misemo mingine ni migeni kabisa masikioni mwa walio wengi. Rais Samia amesikika akisema misemo kama “Ukishindwa Utasaidiwa”, “Nitawapima mabega yenu kwa rula”, “Nikisema naomba si udhalili”, “Ufanyaji kazi mwendo wa Jongoo” na mengine mingi tu. Sayansi ya kutumia misemo na tungo kwenye hotuba ni sayansi ya kitambo sana, na kazi yake kubwa ni kufanya watu wasisahau mapema kile kilichowasilishwa, pia kufurahisha na kuwapa watu fursa ya kutanabahi mambo kwa undani zaidi kuhusu hotuba iliyotolewa kwao.
  1. Kupanda na kushuka kwa sauti.
    Kupanda na kushuka kwa sauti ni moja ya ujuvi alio nao Rais Samia kwenye kuhutubia hadhira. Wataalamu wa masuala ya hotuba wanashauri kuwa hotuba lazima itolewe kwa sauti yenye kupanda na kushuka ili kuvutia hadhira. Si vyema sana kutumia sauti ya juu sana au ya chini moja kwa moja wakati kiongozi anatoa hotuba. Yako maeneo kulingana na ujumbe fulani, sauti inapasa kupanda kutoa msisitizo, na pia yapo maeneo ni lazima kiongozi kupunguza sauti kuzituliza nafsi za wasikilizaji. Rais Samia suala kwenye hili amebobea, sauti yake hupanda na kushuka mwanzo hadi mwisho. Si kila kiongozi, ana kipawa cha namna hii.
  1. Tabasamu na lugha ya Ishara
    Rais Samia mara nyingi hupenda kutabasamu kwenye hotuba zake. Tabasamu ni muhimu sana kwenye kuliteka sikio la msikilizaji, ni ishara ya upendo na amani katika eneo hilo. Kufungua hotuba kwa sauti ya chini, upole na tabasamu usoni, huvuta hamu na hamasa ya mtu kutaka kujua jambo linalotaka kuzungumzwa. Mara nyingi azungumzapo na hadhira barabarani wakati wa ishara zake, hutumia sana ishara za mikono wakati anazungumza. Matumizi ya ishara kwa mujibu wa tafiti ni alama ya mamlaka, kujiamini, ukweli wa maneno na pia njia ya kuiteka hadhira hasa katika matamshi ya mzungumzaji.
  1. Kusita
    Rais Samia ana tabia ya kunyamaza kidogo wakati anatoa hotuba. Kama ni mfuatiliaji, utaona kuna nyakati hunyamaza kwa sekunde kadhaa kisha kuendelea. Kitendo hiki sio cha bahati mbaya kwenye kutoa hotuba, bali ni sayansi inayotumika katika kufunda mahatibu. Kitendo cha kusita kina faida kadhaa, kwanza kufanya hadhira kufikiri juu ya neno la mwisho kuzungumzwa katika ya kusita, ni njia ya kuonesha msisitizo kwenye neno lililopita na pia ni namna ya kurudisha hadhira kwenye mstari. Mzungumzaji anapokuwa anaongea, halafu akasita ghafla, basi hadhira hugatuka na kuanza kusikiliza tena kwa kuwa mara nyingi ukimya katikati ya hotuba si jambo linalotarajiwa na wengi, hivyo kuwafanya wasikilizaji warudishe mawazo yao kwenye kusikiliza zaidi.
error: Content is protected !!