Rais Samia Suluhu Hassan amezindua meli ya kwanza ya uvuvi wa Bahari Kuu ambayo itaiwezesha nchi kuvua samaki waliopo kwenye Ukanda wa Maalum wa Uchumi wa Bahari (EEZ) ambao awali haukuweza kufikiwa kutokana na kukosekana kwa meli ya aina hiyo.
Hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika Aprili 25,2026 kwenye ufukwe wa Makao makuu ya Shirika la Uvuvi (TAFICO) Kigamboni mkoani Dar es Salaam ambapo Rais Samia amesema kuwa hatua hiyo inalenga kukuza fursa za ajira, kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha lishe.
“Niipongeze Serikali ya Japan kwa kushirikiana nasi katika kutengeneza meli hii na kupitia wao kwa kushirikiana na UNDP tutapata boti mbili za kasi ambazo zitasimamia doria ya uvuvi wa bahari kuu,” ameongeza Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha sekta ya Uvuvi kupitia ujenzi wa bandari za uvuvi ikiwemo ya kilwa ambayo imefikia asilimia 97 na Bagamayo ambazo zote kwa pamoja zinalenga kuimarisha uchumi, ajira na usalama wa chakula.
“Sambamba na hilo tutaimarisha mafunzo na tafiti za kitaalam ili kuhakikisha rasilimali za bahari zinasimamiwa kwa ufanisi na misingi endelevu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo,”amesema Rais Samia.
Rais Samia ametoa maelekezo mbalimbali kwa wizara ikiwa ni pamoja na kutunza meli hiyo, kutatua changamoto za wavuvi wadogo zinazohusu mitaji na mazingira ya kufanya shughuli zao, kutoa elimu ya usimamizi wa fedha kwa wavuvi ili fedha wanazopata ziwanufaishe na kutumia sheria na taratibu kwenye usimamizi wa uvuvi endelevu na badala ya nguvu na mabavu.
Akizungumza awali, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Balozi Dk Bashiru Ally Kakurwa amemshukuru Rais Samia kwa jitihada za kuendeleza sekta ya uvuvi nchini ambapo ameeleza kuwa Meli hiyo ni sehemu ya meli nyingine nne zinazotarajiwa kununuliwa na serikali ili ziimarishe uvuvi wa Bahari Kuu.






