Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewataka vijana nchini kurejea katika misingi ya mshikamano na kuacha vitendo vinavyoweza kusababisha migawanyiko katika jamii.
Akizungumza katika Kongamano la UVCCM lililofanyika Tunguu, Zanzibar, Dkt. Samia amesema jukumu la kuendeleza na kuimarisha Muungano wa Tanzania liko mikononi mwa Watanzania wote, hususan vijana wa CCM.
Amesema anajivunia kuona nchi ikiwa imara, yenye amani na utulivu, lakini akaonya kuwa mshikamano wa Watanzania unaanza kulegalega hatua kwa hatua, hali inayopaswa kutafakariwa kwa kina.
“Nawaomba sana vijana, tushikamane. Tukishikamana adui hana nafasi ya kupita, lakini tukikubali kutenganishwa tunampa adui njia ya kupita,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, amekemea matumizi ya maneno na mienendo inayochochea ubaguzi miongoni mwa vijana, akisisitiza kuwa hali hiyo inaweza kuhatarisha umoja wa taifa.
Rais Samia amewataka vijana kupendana, kushirikiana na kulinda amani ya nchi ili Tanzania iendelee kuwa moja na yenye mshikamano imara.



