Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limesema linamsaka mwanamke anayedaiwa kuwatupa vichanga mapacha wa jinsia ya kiume, wanaokadiriwa kuwa na umri wa miezi mitano hadi sita tangu kutungwa kwa mimba.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 27, 2026, katika Mtaa wa Chamwenda, Kata ya Nyasaka, Wilaya ya Ilemela, baada ya polisi kupokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu kuonekana kwa miili ya vichanga hivyo ikiwa imetupwa jalalani.
Katika taarifa yake, Jeshi la Polisi limesema askari walifika eneo la tukio na kufanya uchunguzi wa awali, kisha miili hiyo ikachukuliwa na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure.
“Juhudi za kumtafuta mtuhumiwa na kubaini chanzo cha tukio ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake zinaendelea,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Jeshi hilo limetoa wito kwa mtu yeyote mwenye taarifa zinazoweza kusaidia uchunguzi kuziwasilisha kwa polisi ili kufanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa.


