Rais Samia ataka mpango wa maendeleo wa kuhudumia wananchi mil. 61.7

HomeKitaifa

Rais Samia ataka mpango wa maendeleo wa kuhudumia wananchi mil. 61.7

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ongezeko la idadi ya watu Tanzania ni mzigo kwa Taifa, hivyo lazima iwepo mipango madhubuti ya kuwahudumia watu milioni 61.7.

Idadi hiyo ya Watanzania imetangazwa leo Oktoba 31, 2022 jijini Dodoma na Rais Samia wakati akizindua Chapisho la Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi la 2022 na Mwongozo wa Kitaifa wa Matumizi ya Sensa ya Watu na Makazi wa mwaka 2022.

“Inawezekana idadi hiyo isiwe tatizo la kuhumiza kichwa kwa nchi kama yetu lakini ni mzigo mkubwa kwa Taifa, jamii na uchumi kwa ajili ya kuwahudumia.

“Kuanzia sasa lazima pawepo na mikakati madhubuti katika mpango wa maendeleo ya jinsi ya kuwahudumia watu hao milioni 61.7,” amesema Rais Samia.

Makadirio yanaonyesha kuwa ifikapo mwaka 2025 Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 67.9 na ifikapo mwaka 2050 Tanzania itakuwa na watu milioni151.3.

Aidha, Rais Samia amesema matokeo ya Sensa ya Idadi ya Watu yatumike katika kupanga miradi ya wananchi, bajeti, sekta binafsi na wawekezaji wote wa mipango jumuishi na mendeleo endelevu.

error: Content is protected !!