Madini ya kinywe na adimu kuvutia uwekezaji nchini

HomeKitaifa

Madini ya kinywe na adimu kuvutia uwekezaji nchini

Serikali inatarajia kuvutia uwekezaji wa Dola za Marekani milioni 667 sawa na Sh1.5 trilioni baada ya kuanza kuchimba na kuchakata madini ya kinywe na adimu ambayo yatasaidia kuongeza mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia huku ikiboresha maisha ya wananchi.

Kwa mujibu wa Rais Samia Suluhu Hassan akirejea utafiti wa madini ya kinywe na madini adimu ulioanza mwaka 2000 kupitia kampuni mbalimbaili, hadi sasa kuna mashapu tani milioni 67 yenye wastani wa asilimia 5.4 ya madini ya kinywe yaliyogundulika katika Kijiji cha Chilalo mkoani Lindi ambayo yatachimbwa kwa muda wa miaka 18.

Tani milioni 63 zenye 7.6 ya madini ya Kinywe yamegundulika katika Kijii cha Ipanko, mkoani Morogoro ambayo nayo yatachimbwa kwa miaka 18 huku tani milioni 18.5 zenye asilimia 4.8 ya madini adimu yamegundulika katika Kijiji cha Ngualla mkoani Songwe ambayo uchimbaji wake ni wa miaka 20.

Madini haya ya kinywe na adimu yanajulikana kama madini muhimu ya kimkakati duniani kutokana na uwezo wake wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Yanahitajika sana katika teknolojia mpya za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo hutumika kutengeneza betri za magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki na mitambo mbalimbali,” amesema Rais Samia aliyekuwa akizungumza jana Aprili 17, 2023 Ikulu mkoani Dodoma wakati wa utiaji saini mikataba ya makubaliano kati ya Serikali na kampuni tatu za madini kutoka nchini Australia.

Amesema kutokana na Tanzania kuwa na  madini haya, imekuwa nchi ya kutamaniwa na wawekezaji duniani.

“Katika siku zijazo nchi yetu itakuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji wa madini haya na hivyo kuweza kuvutia uwekezaji mahiri,” amesisitiza kiongozi huyo mkuu wa nchi.

Amesema utekelezaji wa mikataba hiyo utafungua fursa mbalimbali ikiwemo ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua madini hayo hivyo kufaidika na fedha zitakazolipwa na nchi nane jirani zinazoizunguka Tanzania zenye madini hayo.

Serikali itapata kodi, tozo, itafungua fursa za ajira na biashara hasa kwa wananchi walio karibu na migodi ya madini hayo, itasaidia kukuza uwezo wa kitaaluma na kurudisha hisani kwa jamii.

“Kwa mwenendo huu ambao tunajitahidi kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini sekta ya madini itazidi kukua na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.

Ni matarajio yangu kuwa kwamba ifikapo 2025 sekta hii itatimiza lile lengo tulilowekewa kwenye Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025 sekta hii ichangie katika pato la Taifa kwa asilimia 10,” amesema Rais.

error: Content is protected !!