Finland yawaalika wasio na wapenzi duniani kwa safari ya bure ya kutafuta wapenzi

HomeKitaifa

Finland yawaalika wasio na wapenzi duniani kwa safari ya bure ya kutafuta wapenzi

Finland, ambayo mara nyingi hutajwa kuwa nchi yenye furaha zaidi duniani, imewaalika watu wasio na wapenzi kutoka sehemu mbalimbali duniani kushiriki safari ya bure ya kukutana na watu wapya na kutafuta wenzi, itakayofanyika Februari 2027.

Kampeni hiyo inayojulikana kama Finnish Dinner Date imeanzishwa na Bodi ya Utalii ya Finland, Visit Finland. Lengo lake ni kuwafahamisha wageni kuhusu utamaduni wa vyakula vya Finland na kuwapa nafasi ya kukutana na watu wanaoweza kuwa wenzi wao wa kimapenzi.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes, watu 16 wenye umri wa miaka 18 au zaidi watachaguliwa kushiriki safari hiyo itakayofanyika kuanzia Februari 9 hadi 19, 2027.

Wakati wa safari hiyo, washiriki watapata nafasi ya kujifunza kuhusu vyakula vya asili vya Finland, kuonja vyakula mbalimbali vya maeneo tofauti na kushiriki chakula cha pamoja na watu wasio na wapenzi kutoka Finland. Shughuli hizo zitafanyika katika miji ya Helsinki na Tampere.

Baadhi ya vyakula vitakavyotolewa vitatengenezwa kwa kutumia samaki wa porini, matunda ya porini na uyoga unaopatikana katika mazingira ya asili, vitakavyoandaliwa na baadhi ya wapishi maarufu nchini humo.

Watu wenye umri wa miaka 18 au zaidi kutoka nchi yoyote duniani wanaweza kuomba kushiriki, ilimradi si wakazi wa Finland. Mwombaji anatakiwa kurekodi video fupi kwa lugha ya Kiingereza akijibu swali: “Ungeandaa chakula gani kwa ajili ya miadi ya chakula cha pamoja na mtu unayetaka kumfahamu, na kwa nini?”

Baada ya kurekodi video hiyo, anatakiwa kuichapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii kama Instagram, TikTok au YouTube, kwa kutumia alama ya reli #FinnishDinnerDate na kuitambulisha akaunti ya Visit Finland.

Mwisho wa kutuma maombi ni Novemba 10 saa 5:59 asubuhi kwa saa za Finland. Washiriki watakaopatikana watajulikana Desemba 1 kupitia akaunti za Visit Finland za Instagram na TikTok.

Bodi ya Utalii ya Finland italipia gharama zote za safari kwa washiriki watakaochaguliwa, ikiwemo nauli za ndege, malazi, chakula na shughuli mbalimbali watakazofanya nchini humo.

error: Content is protected !!