Wanaume Geita walilia wake zao

HomeKitaifa

Wanaume Geita walilia wake zao

Wanaume mkoani Geita wanaodai kutendewa vitendo vya ukatili na wake zao ikiwamo kupigwa na kunyimwa unyumba wamejitokeza kwa wingi katika dawati la jinsia na watoto kuripoti shida hizo wanazopitia.

Mratibu wa dawati la jinsia na watoto Wilaya ya Geita kutoka Jeshi la Polisi, Sajenti Hidaya Mrisho, aliyasema hayo wakati akitoa mada katika kongamano la wanawake Mkoa wa Geita.

Sajenti Hidaya alisema kuna wakati amekuwa akilengwa na machozi anapopokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya kinababa wanaofika kutoa malalamiko yao kwenye dawati hilo.

“Kumekuwapo na kukosekana kwa ufahamu kwani wengi wanadhani dawati la jinsia na watoto ni kwa ajili ya wanawake na watoto peke yao, wakati dawati hilo ni kwa ajili ya jinsia zote hii inasikitisha sana. Wapo baadhi ya wanaume wanaona aibu kujitokeza , naomba wajitokeze kama wengine walivyojitokeza na kudai wamekua wakipigwa na wake zao pamoja na kunyimwa unyumba,” alisema Sajenti Hidaya.

Aidha, Sajenti Hidaya alisema kuna baadhi ya kina baba wanaoamriwa na wake zao kufua nguo zao za ndani zikiwamo nguo za kujisitiri na kushauri kuwa usawa unapaswa kuzingatiwa kwa kila mmoja kutimiza wajibu na majukumu yake katika familia itasaidia katika furaha, maadili na kujenga familia zenye maadili ya kijamii. 

error: Content is protected !!