Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limewataka wateja wanaokumbana na changamoto za mafundi cherehani kuchelewesha kazi, kutokamilisha nguo au kupotea baada ya kupokea nguo zao, kuwasilisha malalamiko yao katika baraza hilo ili hatua zinazostahili zichukuliwe.
Afisa Sanaa Mwandamizi wa BASATA, Abel Ndaga, amesema hatua hiyo inatokana na malalamiko mengi yanayopokelewa kutoka kwa wateja ambao wamekuwa wakipata usumbufu baada ya kukabidhi nguo zao kwa mafundi na kushindwa kupata huduma kama walivyokubaliana.
Amesema BASATA inalenga kuweka utaratibu utakaowafanya mafundi cherehani watambulike rasmi na kuwajibika kwa kazi wanazofanya. Kwa sasa, baraza hilo linaandaa mfumo wa usajili utakaowajumuisha mafundi wote wa cherehani nchini, wakiwemo wale ambao hawajasajiliwa.
Ndaga ameeleza kuwa usajili huo utasaidia kuinua hadhi ya ushonaji kama taaluma ndani ya tasnia ya ubunifu, kuongeza viwango vya kitaaluma na kuwawezesha mafundi kupata fursa za mikopo ya fedha, vifaa pamoja na msaada wa kisheria.


