Tanzania na Nigeria kuandaa mkutano wa kwanza wa Afya ya Wanawake Afrika mwezi Desemba

HomeKitaifa

Tanzania na Nigeria kuandaa mkutano wa kwanza wa Afya ya Wanawake Afrika mwezi Desemba

Rais Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania kwa kushirikiana na Nigeria itaandaa mkutano wa kwanza wa Afya ya Wanawake Afrika, utakaofanyika Desemba Mosi, 2026.

Amesema mkutano huo unalenga kuimarisha ufuatiliaji wa maazimio ya kisiasa na uwajibikaji katika utekelezaji wa malengo ya kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto, pamoja na kuimarisha maendeleo ya watumishi wa afya na utoaji wa huduma za afya katika ngazi za jamii.

Akizungumza katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, Rais Samia amesema ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za kuendeleza utekelezaji wa vipaumbele vya afya ya uzazi, mama, mtoto mchanga, mtoto na vijana barani Afrika.

Ameeleza kuwa mkutano huo utatoa fursa ya kuendeleza dhamira ya viongozi wa Afrika katika kuhakikisha ahadi zilizowekwa kuhusu afya ya mama na mtoto zinatafsiriwa kuwa hatua zinazotekelezeka na matokeo yanayopimika.

Rais Samia ametoa wito kwa nchi za Umoja wa Afrika kuimarisha umiliki wa mipango ya afya na kuhakikisha mikakati iliyowekwa inatekelezwa kwa ufanisi ili kuboresha ustawi wa wanawake, watoto na vijana katika bara hilo.

error: Content is protected !!