Afisa Mwajiri mbobevu ameleza namna ambavyo husoma barua za maombi ya kazi ya waombaji mbalimbali, na vitu gani anazingatia zaidi kwenye barua hizo. Ameeleza kuwa husoma wastani wa barua 60 kila mwaka zinazotumwa kwenye ofisi yao, hivyo ana uzoefu wa kutosha kujua kizuri na kibaya.
Kwa uzoefu huo ameeleza vitu anavyofanya/ kutazama wakati anasoma barua:
1. Msingi wa Barua
Kitu cha kwanza kutazama ni makosa kwenye barua, na ni rahisi sana kuyaona makosa ya mwandishi kuliko hata yeye mwenyewe. Ufunguzi wa barua unaweza ukawa na tafsiri tofauti kwenye kichwa cha mwajiri, mfano, matumizi ya maneno,”Dear Sir/Madam”, “To whom it may concern”, yanaweza kumfanya mwajiri ahisi kama hukuchukua muda kujiandaa kuomba ajira hiyo, na hujali kufanya kazi mahala hapo.
Kwa sababu, mtindo huo wa uandishi mara nyingi wa kuiga, na hutokana na hisia kwamba uandishi wa namna hiyo mwajiri anaweza kuvutika kukuita kwenye usaili.
Huitaji kutumia maneno kama “Nashuruku kwa muda wako kusoma barua yangu”, huitaji kabisa kwani kusoma ni kazi yake, sio hisani. Ukionekana na unashukuru sana na kutia huruma kwenye barua yako, mwajiri anahisi kama una msongo au matatizo, anashjndwa kuona kiini cha lengo lako kuomba kazi.
Eleza namna gani utafanya kazi na kufikia malengo ya kampuni. Andika barua yenye kuanisha muunganiko kati ya uzoefu wako na mahitaji ya kazi unayoomba. Mweleze mwajiri kwa muhtasari mafanikio yako na namna yanavyotoa tafsiri kwenye kufanikisha malengo ya kampuni/taasisi unayoomba.
2. Maneno ya Ufunguzi
Epuka kuanza barua na maneno kama “Naandika barua hii kuomba kazi kwenye kampuni fulani.” Inaelezwa kuwa waajiri wengi hawapendi kuona sentensi hii, wanaona ni sawa na kumkumbusha kitu anachokijua. Ni kweli, kwani wao wanajua unaandika barua kwanini na wanaijua kampuni unayoomba kazi, kuna haja gani ya kurudia? Inawakera, na huchukua barua nyingine kuendelea mbele. Tazama mifano wanayoshauri itumike kwenye uandishi.
“Ilikuwa ni ndoto yangu kufanya kazi kama mkutubi tangu nikiwa shuleni, namshuru Mama Janeti kwa kunifanya nipende kusoma”
“Mtindo wangu katika uongozi ni rahisi, azma yangu kila siku ni kuhakikisha nakuwa kiongozi bora kwa wengine ambaye hata binafsi ningetamani kufanya nae kazi”
“Miaka mitatu iliyopita kwenye kampuni A niliweza kuongeza mauzo kutoka milioni 50 kwa mwezi hadi milioni 100”..
Mifano hiyo hapo juu, mwajiri anasema lazima aendelee kusoma, na ni rahisi sana kukukumbuka hata asome barua 500, kwani umeanza tofauti na kauli adimu kabisa, epuka sana kuwa wa kawaida.
3. Namna ya kuwasilisha ujuzi wako
Hauhitaji kuandika “Nina ujuzi fulani,” “Nina kipaji kwenye kazi fulani,” “Sasa hivi nasoma kitu fulani.” Lengo sio kuonesha una vigezo kuliko mwingine, ukiandika hivi ni wazi ujuzi wako umeendana kabisa na tangazo la kazi, hivyo ni kawaida kukuta kila aliyeomba kazi anavigezo vyote kutokana na tangazo.
Sasa ili yeye achague mmoja, atalazimika kutazama kitu gani kinawatofautisha zaidi. Kikubwa hapa ni kujitahidi kuwa tofauti kadiri uwezavyo, ili akukumbuke.
Unaweza kuandika hivi, “Kama tutakuwa kwenye mkutano video call/projector itasumbua, mimi sio mtu wa kusubiri “IT” aje, nitaingia mwenyewe uvunguni kutazama kama kila kitu kiko sawa”.. Kauli hii itaonesha ujuzi wako, uwajibikaji na utakuwa tofauti zaidi ya wengine.
Zingatia: Kabla hujatuma barua, hakikisha kila ulichoandika, kinaweza kumfanya mwajiri akukumbuke, epuka kuinga barua za google, kila mtu anaiga huko, kuwa tofauti ukumbukwe.