Gazeti la Raia Mwema lasitishiwa leseni ya uchapishaji na usambazaji

HomeKitaifa

Gazeti la Raia Mwema lasitishiwa leseni ya uchapishaji na usambazaji

Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari, Gerson Msigwa kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 9(b) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016 ameamua kusitisha kwa muda wa siku thelathini (30) leseni
ya uchapishaji na usambazaji wa gazeti la Raia Mwema kuanzia kesho tarehe 06 Septemba, 2021.

 

Kwa mujibu wa barua iliyotolewa leo na Idara ya Huduma za Habari, Maelezo, uamuzi wa kusitisha leseni ya gazeti la Raia Mwema unatokana na mwenendo na mtindo wa uandishi wa habari na makala ambao kwa kiasi kikubwa unakiuka misingi ya maadili ya taaluma ya habari kwa kufanya upotoshaji wa mara kwa mara wa taarifa na uchochezi wa bayana. Kwa kufanya hivyo gazeti hili limekiuka masharti ya leseni liliyopewa jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linaweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuleta chuki miongoni mwa jamii na vilevile
kuwafanya wananchi waichukie Serikali na viongozi wake.

 

Mifano michache ya habari na makala ambazo kwa kiasi kikubwa zilikiuka masharti ya leseni ambayo imeanishwa katika barua hiyo ni pamoja na gazeti toleo Na.844 la tarehe 21 Agosti, 2021 lililochapisha habari iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Maumivu mapya 17”. Gazeti la Raia Mwema toleo Na.853 ukurasa wa 1 na kuendelea ukurasa wa 3 na wa 4 liliandika habari yenye kichwa kisemacho “Hamza wa CCM hatari,“. Gazeti hili lilitaka kuuaminisha umma kuwa Hamza ni mwanachama wa CCM ama kiongozi wa CCM (Chama Tawala) bila kuwa na uthibitisho usioacha shaka yoyote, jambo ambalo linaweza kuleta chuki miongoni mwa wanachama wa CCM na makundi mengine ya jamii huku likijua kuwa kuandika habari hiyo ni kinyume
na kifungu cha 50(1) (b),(d), (e) na kifungu cha 52(1) (e) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016.

Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya 2016, ikiwa wahusika hawataridhika na uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari, wanayo haki ya kukata rufaa kwa Waziri mwenye dhamana ya Habari ndani ya siku thelathini (30) tangu siku ya uamuzi huu.

 

 

error: Content is protected !!