Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa amebainisha hayo jana tarehe 20 Septemba 2021 wakati akizungumza na vyombo ya habari Jijini Dodoma. Msigwa amesema kuwa Tanzania imesajili miradi mipya ya uwekezaji 133 yenye thamani ya jumla ya Dola Bilioni 2.9 sawa na shilingi trilioni 7 za kitanzania kati ya Machi na Agosti 2021.
Msigwa ameongeza kuwa miradi mingi kati ya hizo ni kwenya sekta ya kilimo, ujenzi, biashara, nishati, miundombinu, usafirishaji, utalii na masuala ya fedha. Msigwa amesema kuwa matokeo hayo chanya yamefanikiwa kutokana na Serikali ya awamu ya Sita kufanya kukifanya kituo cha uwekezaji nchini (TIC) kuwa kituo cha pamoja cha kutolea huduma.
Mafanikio hayo makubwa yamekuja baada ya Kituo cha uwekezaji nchini kujumuisha taasisi 12 za Serikali chini ya mwamvuli mmoja kurahisisha utoaji wa huduma za uwekezaji. Baadhi ya taasisi zilizojumuishwa ni TANESCO, BRELA na TRA. Pia Serikali imeongeza dirisha ambalo litawafanya wawekezaji kuweza kusajili uwekezaji kwa njia ya mtandao.
Msigwa amesema kuwa maeneo 273 ya ardhi yamepimwa ambayo yana ukubwa wa hekta 159,721 katika maeneo mbalimbali nchini yatakayopunguza kero kwa wawekezaji. Miradi 26 kati ya 133 imesajiliwa na Watanzania binafsi, huku 34 sawa na 25.56% ni miradi iyoingiwa kwa ubia.
Msigwa alitaja moja ya mradi ambao unatekelezwa kwa sasa ni kiwanda cha mbolea jijini Dodoma chenye thamani ya dola milioni 180 (Sh. 423 Bilioni). Kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha tani 500,000 za mbolea kwa mwaka na uwezo wa kuajiri wafanyakazi 3000.
Msigwa pia amesema Kiwanda kingine ni cha S. J. Sugar Company ambacho kinahusika na kutengeneza Sukari katika kijiji cha Kitere mkoani Mtwara. Kiwanda hicho kiko katika hatua za mwisho za umiliki wa ardhi kabla ya kuanza uzalishaji rasmi.
Aidha Msigwa amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anaalika wawekezaji zaidi katika bidhaa mbalimbali na uwekezaji ambao utakuwa na maslahi kwa pande zote, hivyo Rais Samia anaalika wawekezaji kuipa kipaumbele Tanzania kwenye uwekezaji.
“Tunawahakikishia wawekezaji soko la uhakika nchini kutokana na kuongeza kwa idadi ya watu, na pia kupita Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Nchi za SADC” – Alisema Msigwa