Serikali kupitia Waziri wa Nchi, ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama imetoa taarifa fupi kuhusu maandalizi na taratibu za maziko ya aliyekuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, William Tate Ole Nasha (Mb) ambaye alifariki Septemba 27, 2021 akiwa nyumbani kwake maeneo ya Medeli jijini Dodoma.
Waziri Mhagama ameeleza kuwa kwa sasa Serikali inaandaa utaratibu wa kumuaga marehemu kitaifa siku ya Alhamisi majira ya saa 5 asubuhi huku maziko yakitarajiwa kufanyika Ijumaa na Jumamosi kijijini kwa Marehemu Ole Nasha.
Waziri Mhagama amesema kuwa hayo ni maamuzi ya kikao cha awali kilichofanywa ila kutakuwa na kikao kingine na endapo kutakuwa na mabadiliko basi watatoa taarifa kwa umma. Pia Waziri Jenista amewashukuru Watanzania kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kipindi hiki cha maombolezo huku akiwataka kuendelea kuwa watulivu.